December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amekutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini kwa lengo la kuwafahamisha  kuhusun mifumo mbalimbali serikalini iliyojengwa ili kuboresha utumishi wa umma.

Akizungumza na viongozi hao   katika  kikao kazi cha kuwajengea uelewa kuhusu mifumo hiyo Mhagama amesema, hatua hiyo itawawezesha kwenda kuwaelimisha watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao bila shuruti.

“Katika kusimamia rasilmali zote nchini tulizonazo,mipango ya maendeleo,mipango fedha  na mipango mingine,na tukiweza kufanya kazi kwa pamoja ,tukaelewana,tukabainisha changamoto tulizo nazo lakini tukazingatia sheria na taratibu mwisho wa siku tutakuwa tumetoa mchango mkubwa sana katika maendeleo na ustawi wa Taifa letu.”amesema Mhagama

Baadhi ya viongoiz wa vyama vya wafanyakazi wakiwa katiia kikao kazi na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama

Amesema  serikali imekuwa ikifanya mabadiliko mengi yakiwemo ya kimfumo pamoja na ajira ni chachu ya maendeleo hata katika vyama vya wafanyakazi .

“Kwa mfano wiki ijayo Mheshimiwa Rais ametoa kibali cha kuajiri watumishi 32,000 ,hivi hapo na nyie vyama vya wafanyakazi mtakuwa mmeula kwa kuwa pia atakuwa amejenga nguvu ya kutosha kwa wafanyakazi kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi na mambo mengine kupitia wananchama yataongezeka na kuimarika .”amesema na kuongeza kuwa

“Ndio maana Ofisi yangu tumepokea maelekezo ya Rais ya kuihakikisha tunaweka mifumo imara itakayotuwezesha pia kufikia mipango mbalimbali ya maendeleo kutokana na utendaji mzuri kwa watumishi wa umma.”amesema

Baadhi ya viongoiz wa vyama vya wafanyakazi wakiwa katiia kikao kazi na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama

Ametaja mifumo iliyojengwa katika ofisi yake kuwa ni pamoja na  Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) uliolenga kuondoa changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendajikazi wa watumishi wa umma.

“Mfumo mpya wa PEPMIS utakuwa ni wa kielektroniki na utaondokana na matumizi ya makaratasi,pia utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji wa watumishi..,pia mfumo huu pia utahamasisha uwajibikaji wa hiari na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa watumishi.”

Ameutaja mfumo mwingine kuwa ni Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi (PIPMIS) mfumo ambao amesema ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja huku akisema mfumo wa huo wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na taifa kwa ujumla.

Amesema,Ofisi ya Rais Menejementi ya Utumishi wa Umma imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA inayohusu uendeshaji wa Serikali wa kila siku na kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa umma.

Mhagama amesema,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kujenga Mfumo wa Sema na Waziri , Mfumo wa e-mrejsho, Mfumo wa Dawati la Huduma kwa Mteja maarufu kama UTUMISHI Call Centre ,Mfumo maalum wa Tathmini ya hali ya Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal).

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu)  Joyce Ndalichako amebainisha kuwa pamoja na juhudi za serikali za kupima utendaji kazi serikalini  Rais amelekeza ushirikishwaji wa Vyama vya Wafanyakazi ili waendelee  kuwa daraja kati ya waajiri na Wafanyakazi kwa kuchochea na kuhimiza utamaduni kwa Wafanyakazi kudai haki na kutimiza wajibu wao.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu imeendelea kutekeleza maagizo ya  Rais kwa kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji wa Vibali vya Kazi kwa raia wa kigeni ambao  umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku za kazi 14 hadi siku 7.

Naye Rais wa shirikisho la wafanyakazi nchini TUCTA Tumaini Nyamhokya  amesema,wao kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanachopenda ni wafanyakazi kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na kwamba kinachotakiwa mifumo isiwe ni ya kunyanyasa wafanyakazi hasa kuwatumikisha zaidi ya muda wa kazi na bila mwajiri kutambua hilo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (CWT) Deus Seif  amesema,mfumo wa awali wa OPRAS ulikuwa na changamoto nyingi hasa kwa walimu huku akisema anaamini mfumo unaokuja wa upimaji kazi utaweka mazingira sawa kwenye kupima utendaji kulingana na mazingira ya halisi na hivyo kufanya watumishi wa umma waufurahie utumishi wao.