Na David John,Timesmajira online
KATIBU wa Mgodi wa Mahina uliopo Kijiji cha Nyakafulu Kata ya Nyakafulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Isaya Ngwijo Amesema kuwa mgodi huo umeweza kutoa fursa za ajira zaidi ya 300 tangu ulipoazishwa mwaka 2019.
Amesema kuwa fursa hiyo ya ajira inatokana na ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka serikalini pamoja na mamlaka zinazowasimamia kwenye sekta hiyo ya madini ikiwepo Tume ya Madini yenyewe.
Ngwijo ameyasema hayo Juni 15 wilayani humo mara baada ya waandishi wa habari kutembelea mgodini hapo kwa lengo la kujifunza namna shughuli za madini zinavyofanyika.
Amesema kuwa ajira hizo zimeweza kuzalishwa kupitia makundi tofauti tofauti wakiwemo vijana na wanawake pia mgodi huo licha ya kutoa ajira umekuwa ukichangia huduma za kijamii na mchango wa moja kwa moja kwenda serikali kuu na halmashauri.
“Tumekuwa tukishiriki katika ujenzi wa shule,vyoo, madarasa na zahanati, tumekuwa tukijitoa kama mgodi na tumekuwa tukifanya hivyo ili kusapoti juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi,”amesema Ngwijo.
Akizungumzia malengo ya Mgodi amesema kuwa mpango wao kama mgodi wa Mahina ni kuwa na uchimbaji wa kisasa na mbele zaidi ni kuwa na taasisi kubwa inayomilikiwa na wazawa ili kuweza kurahisisha shughuli za uchimbaji kama ilivyo kwenye migodi mingine mikubwa.
“Mara nyingi tumekuwa kama mfano Kwa maana kwamba hata ukiangalia namna tunavyoendesha mgodi,tumekuwa kisasa zaidi na hata maeneo yetu ya uzalishaji yanavyoonekana tumekuwa tukitumia uzalishaji wa kisasa.”amesisitiza Ngwijo.
Pia amefafanua kuwa lengo lingine ni kuwa na teknolojia ya kisasa,kuongeza uzalishaji wenye tija na kuongeza pato la serikali ili kutengeneza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Kuhusu changamoto,amesema kuwa ni kawaida kwenye sekta hiyo lakini ni changamoto ya mitaji kwa wachimbaji na kubwa zaidi kumekuwa na ugumu kuzifikia taasisi za kifedha ili kuweza kukopesheka kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Hata hivyo kutokana na juhudi za serikali za kuwaunganisha wachimbaji kwenye sekta za kifedha wameaza kuaminika na taasisi mbalimbali kwa kushirikiana bega kwa bega na wachimbaji wadogo lakini kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye eneo hilo ili fursa za kukopesheka ziongezeke.
Akizungumzia mchakato wa uazishwaji wa Benki ya Wachimbaji amesema kuwa benki hiyo itakuwa mkombozi kwasababu mifano ipo kwa baadhi ya sekta wamekuwa wakifanya vizuri baada ya kuwa na taasisi zao za kifedha.
Amesema kuwa pakiwepo na taasisi kama hiyo inakuwa na fursa ya kuona changamoto za moja kwa moja zinazohusu wachimbaji madini hivyo inakuwa rahisi zaidi kwa benki mahususi kama hiyo kuweza kugundua mahitaji gani ambayo wachimbaji wa kati na wadogo wanakuwa nayo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua