January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia awaasa wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano kuwa chachu ya kudumisha amani,utulivu nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameitaka Jumuiya ya Maridhiano hapa nchini kuwa chachu ya kudumisha amani iliyopo nchini bila kujadili tofauti za dini miongoni mwa jamii.

Jumuiya ya Maridhiano imefanya maadhimisho ya Siku ya Maridhiano iliyolenga kuelimisha jamii kuhusu kudumisha amani ,upendo na mshikamano Maadhimisho ambayo yameenda sambamba na utoaji Tuzo kwa viongozi wa Serikali na viongozi wa Dini walioshiriki kikamilifu katika kuhakikisha amani na Utulivu vinaendelea kuwepo nchini wakiongozwa na Rais Samia .

Vile vile maadhimisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa vitabu vilivyoandikwa na watanzania wapenda amani ambavyo vimelenga kuelimisha jamii juu ya kudumisha amani iliyopo nchini ambapo majina ya vitabu hivyo ni ‘Nani atasalimika amani ikitoweka’na ‘Fahari ya afrika amani ya Tanzania.’

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano mkoa wa Dodoma Askofu Dkt.Evance Chande akipokea tuzo ya mchango wake wa kudumisha amani nchini

Akizungumza kwa niaba yake katika Maadhimisho hayo ,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema,viongozi wa dini katika Jumuiya hiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kuonyesha mfano wa kupendana na kuheshimiana licha ya kuwa na tofauti ya dini zao lakini pia kukemea pale panapoonekana pana viasharia vya unjifu wa amani.

“Nitashangaa kuona kiongozi wa dini anakuwa wa kwanza katika kutoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani au kunyamaza pale wanapoona hali hiyo,ninyi ndio chachu mnaotakiwa muonyeshe mnayoyahubiri kwenye Jumuiya hii kwa vitendo.”alisema Masauni na kuongeza kuwa

Mhandisi Masauni ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuimarisha misingi ya amani upendo ,kuvumiliana na kuheshimiana hasa katika mambo tunayotofautiana katika dini huku akisema misingi hiyo ikiimarishwa itadumu vizazi na vizazi.

Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano wakifuatilia jambo kwenye maadhimisho ya siku ya Maridhiano

Pia Waziri Masauni amempongeza Waziri mkuu Mstaafu ambaye pia ndiye mlezi wa Jumuiya hiyo Mizengo Pinda kwa wazo la kuasisi Jumuiya hiyo tangu mwaka 2014 na kisha kusajiliwa mwaka 2016 na  kudumu mpaka sasa na inaendelea kuimarika kadri siku zinavyosonga mbele.

“Nataka niwahakikishie serikali itafanya kila linalowezeka kuhakikisha Jumuiya hii  na zote zenye nia njema kwa nchi zinapata msaada ili ziweze kutimiza malengo yake ya kuisadia Serikali kuhubiri amani na utulivu nchini.”

Hata amesema pamoja na mafanikio ya kudumisha amani na utulivu wa nchi lakini bado kuna changamoto ya matukio ya mauaji ambayo yanahitaji Jumuiya kushirikiana na Serikali katika kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo huku akitolea mfano mauaji yaliyohusisha vifo vya watu watano wa familia moja yaliyokea wilaya ya Bahi mkoani Dodoma hivi karibuni.

Masauni ametoa wito kwa kwa viongpozi wa Jumuiya hiyo kuimarisha mahusiano lakini pia kuifanya Jumuiya hiyo kuwa daraja daraja kati yake na wananchi na Serikali kwa ujumla.

Miongoni mwa wajumbe wa Jumuiya ya Maridhiano wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Maridhiano

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo  Taifa Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum amesema Jumuiya hiyo imesambaa katika mikoa 28 hapa nchini huku akisema kila mkoa unaadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali p[amoja na kuchangia damu ili kuokoa vifo vya mama wajawazito na watoto.

Aidha amesema Jumuiya hiyo itaendelea kulaani mauaji yote pamoja na vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani ili kupunguza kama siyo kumaliza kabisa vitendo hivyo.

Dkt.Salum ametoa wito kwa watanzania kuendelea  kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kudumisha amani ili maendeleo ya nchi yapatikane kwa haraka.

Kwa upande wake Mlezi wa Jumuiya hiyo Waziri Mkuu Mstaafu Pinda amewataka watu wote waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa mabalozi wa kuhubiri amani,upendo,utulivu na kuvumiliana.

Jumuiya ya Maridhiano kwa mara ya kwanza imesherekea Siku hiyo tangu kuanzishwa kwake hapa nchini Machi 3, 2016 ambapo maadhimisho hayo yatakuwa ni endelevu kwa kuadhimishwa Machi 3,ya kila mwaka.