Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kuachiwa kazi nzito na mtangulizi wake hayati Dkt.John Magufuli,atahakikisha anatekeleza mawazo na miradi yote ilianzishwa naye huku akisema miradi hiyo huwa inamfanya anasikia sauti ya mtangulizi wake huyo ikimwambia kuhusu miradi mbalimbali ya ujenzi pamoja na Dodoma kuwa Makao Makuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa barabara ya mzunguko katika jiji la Dodoma,Rais Samia amesema,atahakikisha anatekeleza kwa ukamilifu miradi yote iliyoasisiwa na mtangulizi wake huyo.
“Mwenzenu siku kama ya leo, mimi mwenzenu huwa nasikia sauti ya mtangulizi wangu hayati Dkt.John Pombe Magufuli ananimabia kuhusu miradi hii ,kuhusu Dodoma kuwa Makao Makuu na kuhusu mambo mengi, na leo hii nimesimama hapa kuweka jiwe la msingi la mradi huu ,
“Lakini waswahili wanasema ukiona vyaelea ujue vimeundwa kwa bahati nzuri muundaji wa suala hili aliyetekeleza maono ya Baba wa Taifa kuhamia Dodoma,akataka kuipanga Dodoma kwa bahati mbaya Mungu amemchukua mapema,lakini aliniachia kazi nzito na nimeahidi mawazo yote aliyoyaanzisha nakwenda kuyatekeleza kikamilifu,
“Na Sehemu hii ni moja kati ya mawazo aliyoyaanzisha tunakwenda kutekeleza kama alivyotaka.”amesema Rais Samia
Kiongozi huyo wan chi ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanautuna mradi huo pindi utakamilika pamoja na miradi mingine kwani Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Mbarawa Mnyaa amesema,lengo la barabara hiyo ni kuchepusha magari yanayosafiri kupitia ushoroba wa kati na ule wa barabara Kuu ya Trans Africa kutoka captown Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri, yasipite katikati ya jiji la Dodoma ili kupunguza msongamano wa magari .
“Kwa kuwa shoroba hizi mbili zinaungnisha nchi yetu na nchi nyingi Barani Afrika hasa majirani zetu wa Kenya Uganda,Ruanda,Kongo na Malawi Serikali ikaona kuna umuhimu wa kujenga barabara ya mchepuo ili kuondosha usumbufu ambao unatokea kutokana na msongamano wa magari katika jiji la Dodoma.”amesema Profesa Mnyaa
Aidha amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hii kutaongeza kasi ya maendeleo ya mkoa wa Dodoma na mikoa jirani ikiwemo kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kuingia na kutoka nje ya jiji la Dodoma ,kukuza na kuchochea katika sekta ya kilimo na viwanda ,kupanua na kurahisisha huduma za kijamii hasa katika sekta za maji, elimu na afya .
Vile vile utafanya jiji la Dodoma kuwa kivutio kwa wawekezaji wa nje na ndani na nchi na hivyo kuongeza fursa mbalimbali za kiuchumi kwa mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla.
Ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ushirikiano wa dhati na Tanzania ambapo mpaka sasa zaidi ya kilomita 1914.8 za sekta ya ujenzi wa barabara pekee zimepata ufadhili wa zaidi ya shilingi trilioni 2.458 kutoka Benki hiyo.
Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt.Dkt .Akinumwi Adesina amempongeza Rais Samia kwa kuweka jiwe la msingi wa barabara hiyo lakini pia amempongeza kwa kuendeleza kazi kubwa aliyoianzisha mtangulizi wake Hayati Dkt. Magufuli.
Awali Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Rogatus Mativila amesema,katika mradi wa ujenzi wa barabara hiyo Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa kiasi cha shilingi bilioni 412 na serikali ya Tanzania itagharamia shilingi bilioni 79.91 huku akisema katika mradi huo jumla ya kilomita 112.3 zitajengwa kwa lami.
Aidha amesema tayari Serikali imeshalipa fidia kwa kiasi cha shilingi bilioni 16.239 kwa wananchi walioathiriwa na mradi huo.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini