Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbeya imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani ya Sh. Bilioni 7.9 katika mwaka wa fedha 2025/2026, sawa na asilimia 101 ya makadirio ya bajeti, na hivyo kuvuka lengo la kukusanya Sh. Bilioni 7.8.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Aidda Haule, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato, ushirikiano wa wananchi pamoja na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa fedha.
Amesema mapato hayo yametokana na sekta mbalimbali zikiwemo biashara, viwanda na uwekezaji, kilimo, mifugo na uvuvi, afya, ujenzi na miundombinu, pamoja na mapato fungwa ya iCHF, NHIF, kodi ya majengo na michango ya wananchi katika vijiji na kata.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichopokea taarifa ya utekelezaji wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, amesema sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji imevuka lengo kwa ukusanyaji wa ushuru wa leseni za biashara uliofikia asilimia 118, sawa na Sh Milioni 228.
Amesema sekta hiyo kwa ujumla imekusanya Sh. Milioni 248 hadi Aprili 30, 2026 kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo ushuru wa nyumba za wageni, leseni za vileo, ada za uwakala wa LATRA na usajili wa biashara.
Katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, amesema zao la parachichi limeongoza kwa mapato baada ya kukusanya Sh. Milioni 42.6 sawa na asilimia 142 ya lengo, huku kahawa ikichangia zaidi ya Sh. Milioni 846 sawa na asilimia 130.
Aidha, amesema ushuru wa huduma umeingiza shilingi milioni 678, ushuru wa maegesho na stendi Sh. Milioni 119, huku mapato ya upangishaji vyumba yakifikia Sh. Milioni 178 sawa na asilimia 86 ya lengo.
Kwa mujibu wa Sheria ya fedha za serikali za mitaa sura ya 290 pamoja na mwongozo wa usimamizi wa mapato ya ndani wa TAMISEMI, halmashauri zinatakiwa kuongeza vyanzo vya mapato na kuhakikisha mifumo ya ukusanyaji inaendeshwa kwa uwazi na ufanisi ili kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo kwa wananchi.

More Stories
Wizara,TPSF kuongeza ushiriki kongamano la kiswahili
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewaÂ
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini