January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ZSSF, WCF kushirikiana fidia kwa wafanyakazi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw. Nassor Shaaban, amesema, Mfuko huo uko mbioni kuanzisha SKIMU ya kulipa Fidia kwa mfanyakazi atakayeumia kazini kama ilivyo kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao unatoa huduma hiyo kwa upande wa Tanzania Bara.

Bw. Shaaban ameyasema hayo wakati wa Kongamano la Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lililofanyika pembezoni mwa Maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyamanzi, Zanzibar.

Maonesho hayo ambayo ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yalianza Januari 10, 2024 na yatafikia kilele Januari 19, 2024.

“Katika utayarishaji wa kuanzisha Mafao (skimu) haya ya mfanyakazi atakayeumia kazini, tumekuwa tukishirikiana sana na wenzetu wa WCF ili kupata uzoefu kutoka kwao ambao, wenzetu wana uzoefu wa miaka mingi na wanasifika kwa kutoa mafao mazuri,” amefafanua Bw. Shaaban.

Amesema, tayari wamepatiwa elimu, uzoefu, sheria na kanuni, zinazosimamia masuala ya fidia kwa wafanyakazi, ili na wao waweze kufanya matayarisho mazuri ya kuanzisha chombo kama WCF.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema, Mfuko huo umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake katika kulipa fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na nchi za Afrika

“WCF imekuwa Mfuko wa kuigwa barani Afrika, ukanda wa SADC na Afrika Mashariki, na kama uzoefu huu tunausambaza katika nchi hizo, tumeona ni vema uzoefu huu pia tuweze kuusambaza kwa ndugu zetu wa Zanzibar na ndio maana tumekua na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha na wao wanafikia azma yao ya kutoa fao hilo,”  amefafanua Dkt. Mduma.

Aidha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, amesema, wananchi wana matumaini makubwa ya kuona ushirikiano wa Taasisi za Umma za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zile za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, unaleta tija katika maisha yao.

“Maendeleo ya nchi hii yanapitia katika mikono yenu, katika taasisi zenu, mashirikiano haya yaonyeshe kwa uwazi kwa wannachi kama ambavyo wameanza kusema kwenye ameneo mengi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi, zimekuwa zinajibu mahitaji na kiu ya Watanzania kila sehemu.” Amefafanua.

Kwa upand wake, Mwenyekiti wa Wakuu wa Taasisi za Umma za Serikali ya Jmahuri ya Muungano wa Tanznaia, Bi. Latifa Khamis, ambaye pia ni Mkuurgenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), amesema, pamoja na mambo mengine, kongamano hilo lina lengo la kuwawezesha wakuu wa taasisi za SMT na SMZ kubadilishana uzoefu na kujadiliana namna ya kushirikiana baina ya taasisi wanazoziongoza.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw. Nassor Shaaban wakati wa Kongamano la Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tnazania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwenye viwanja vya Namanzi, Zanzibar

Dkt. Mduma (katikati) na Bw. Shaaban (kulia) wakiwa kwenye kikao hicho

Kutoka kushoto Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mkuu NSSF, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma na Mkurugenzi wa Uendeshaji ZSSF, Bw. Nassor Shaaban, wakiwa kwenye kikao hicho.

Kutoka kushoto Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga, Mkurugenzi wa Uendeshaji ZSSF, Bw. Nassor Shaaban, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, Mkurugenzi Mkuu PSSSF, CPA. Hosea Kashimba na Mkurugenzi Mkuu NSSF, Bw. Masha Mshomba,  wakiwa kwenye picha ya pamoja.