June 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ZOLA yajipanga kupeleka Nishati Safi kwa Watanzania, yaunga Mkono Juhudi za Rais Samia

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Arusha

KAMPUNI  ya ZOLA  inayojishughulisha na usambazaji wa mitambo ya umeme wa jua, imesema imejipanga kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha Tanzania inahamia kwenye matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha wakati wa maonesho ya Karibu-Kilifair 2025 Mwakilishi wa kampuni hiyo, Priscar Mbise, amesema ZOLA imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafahamisha wananchi juu ya bidhaa zao za umeme wa jua, ambazo zimebuniwa kusaidia Watanzania wa kila hali ya kiuchumi kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuchangia uhifadhi wa mazingira.

“Tunatoa huduma ya mitambo ya umeme wa jua inayopatikana kwa gharama nafuu kuanzia shilingi 600 kwa siku, jambo linalomuwezesha kila Mtanzania kumudu kupata nishati safi. Pia tunatoa dhamana (warranty) ya hadi miaka sita kwa mitambo hii,” alisema Mbise.

Mbise alieleza kuwa kampuni hiyo ambayo Makao Makuu yake yapo jijini Arusha , pia inafunga mitambo mikubwa ya umeme wa jua kwenye taasisi kama hospitali, shule, hoteli na viwanda. Alitoa mfano wa hospitali ya Mount Meru jijini Arusha, ambako tayari wameshafunga mitambo katika wodi ya mama na mtoto.

“Tunayo mitambo mikubwa kuanzia 5KVA hadi 25KVA inayoweza kutumika katika maeneo makubwa kama hospitali na viwanda, na tunaiuza kwa bei nafuu kabisa ili kila taasisi iweze kuhamia kwenye nishati safi,” aliongeza.

Mbise amesema nishati ya jua ni salama, rafiki kwa mazingira na ya uhakika hata kwa wale wasiounganishwa kwenye gridi ya Taifa, kwani inaweza kuendesha vifaa vyote vya umeme bila usumbufu.

“Kampuni ya ZOLA inatoa huduma kwa sekta mbalimbali kama elimu, afya, utalii na wananchi wa kawaida. Tunaamini juhudi zetu zinaenda sambamba na dira ya Rais Samia ya kuhakikisha Tanzania inatumia nishati safi ifikapo mwaka 2030,” amesema Mbise

Amewataka Watanzania kuendelea kujifunza kuhusu teknolojia hiyo  ZOLA na kuitumia kwa manufaa yao binafsi na ya Taifa kwa ujumla.