November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zoezi la chanjo awamu ya pili UVIKO Mkoa wa Tanga halifanyi vizuri

Na Hadija Bagasha Tanga,

Zoezi la uchanjaji wa chanjo ya Uviko-19 awamu ya pili katika Mkoa wa Tanga halifanyi vizuri kutokana na watumishi wa afya ambao ndio wahamasishaji wa chanjo hiyo hawajachanja.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Pili Mnyema wakati warsha ya kamati ya afya na uzinduzi wa mradi wa kuongeza muitikio wa kuchanja chanjo ya Uviko -19 iliyofanyika jijini Tanga.

Katibu tawala huyo amesema watumishi wengi ambao ndio vinara wa kuhamasisha watu wengi, wao bado hawajachanja na hivyo kushindwa kutoa elimu sahihi na kushawishi watu kuona umuhimu wa kuchanja kwa lengo la kujikinga na virusi vya Uviko -19.

Alisema watumishi wa afya kutokuwa na utayari wa kuchanja chanjo ya Uviko-19 imekuwa ni moja ya changamoto inayopelekea kiwango cha uchanjaji kuwa chini.

Mnyema amesema awamu ya kwanza ya utoaji wa chanjo walichanja watu 23,539 huku dozi ya pili wakichanja watu 2400 takwimu ambazo ni ndogo hivyo lazima wawe na mkakati wa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kupata chanjo hiyo.

“Watumishi kutokuwa na utayari wa kuchanja hili ni tatizo huwezi kuwa mgamasishaji ikiwa wewe mwemyewe hujachanja viongozi kaongeeni na watumishi hawa kwamba na sisi tuna jukumu la kuchanja, “alibainisha Katibu Tawala Mnyema.

Mnyema amesema licha ya changamoto hiyo ya watumishi wa afya kutokuwa na utayari wa kuchanja lakini pia baadhi ya changamoto nyingine zilizopelekea mkoa huo kuwepo kwenye orodha ambayo haifanyi vizuri kwenye zoezi la chanjo awamu ya pili ya inatokana na ushiriki mdogo wa baadhi ya viongozi wa dini na kisiasa kuanzia ngazi ya vijiji kwenye uhamasishaji.

Mnyema amesema ili waweze kufanikiwa ni lazima kwenye uhamasishaji wapate elimu na kueleza kwenye kundi hilo kuna umuhimu mkubwa kundi hilo liingizwe kwenye uhamasishaji huo kwasababu viongozi wa dini wana kundi kubwa la watu wanaloliongoza.

Pia amesema wenyeviti na watendaji wa mitaa, vijiji nao wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu kubwa la kuhamasisha zoezi hili ili waweze kuunganisha nguvu za pamoja na kuweza kufanikiwa kwenye zoezi hilo.

Awali akifungua warsha hiyo mkuu wa mkoa Tanga Adam Malima amesema kuwa kuwa watu wanaokataa chanjo hiyo wana matatizo kwani serikali na wataalamu wamejiridhisha vya kutosha kuwa chanjo ni salama.

“Twendeni tukatengeneze mkakati wa kuwaelimisha watu tusiwatishie tuwaeleze watu wakichanja wanapopata homa wasiwe na wasiwasi kwani hata chanjo za watoto ziko hivyo hivyo wanapochanja wanapata homa kidogo lakini pia niwaagize muwaweke ndani watu wanaowadanganya wenzao kuhusu chanjo, “alisistiza RC Malima.

Aidha Malima amelitaka Shirika la AMREF pindi wanapokwenda katika jamii kwajili ya zoezi hilo la chanjo washirikiane na watu wanaowakuta kwenye maeneo husika ikiwemo NG’O s.

“Kikao hiki kimeagiza asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya kutoa chanjo wapewe ushirikiano na wakurugenzi wasikwame lolote ili kuwafikia wananchi, “amebainisha Malima.

Hata hivyo Malima amewasisitiza watumishi wa afya kuendelea kuwakumbusha wananchi kuwa siyo kwamba ukichanja hupati maambukizi ya Covid bali ukichanja inasaidia hata ukipata maambukizi hauwezi kushambuliwa zaidi na maradhi.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka wizara ya afya mpango wa Taifa wa chanjo Pricila Kinyuli amesema mpango wa serikali ni kufikia asilimia 60 ya watanzania kuchanja na kwamba katika dozi ya pili ya chanjo unapochoma unatakiwa kukaa siku 28 na kisha kwenda kuchanja nyingine ili dozi iwe imekamilika.

Naye mwakilishi wa mkurugenzi nkuu wa shirika la Amref Tanzania Dkt. Ritha Mutayoba amesema Mkoa Tanga umekuwa ni wa kihistoria kwani wamekuwa wakifanya kazi kwenye maeneo mengi ikiwemo Handeni na Kilindi.

Amesema wamekuwa wakiweka jitihada ambazo wamekuwa wakitoa mara baaday a kisa cha kwanza kutangazwa Tanzania mwaka jana kwa wepesi walifanya utaratibu wa kutafuta rasilimali fedha kuanzia miradi mahususi inayosaidia na serikali kudhibiti mlipuko.

Mganga Mkuu wa Mkoa Tanga Jonathan Budenu amesema Mkoa wa Tanga umepangiwa kuchanja takribani watu milioni 1.5 ambapo mpaka sasa wanaelekea kufikia watu elfu 50.