December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zodo: upatikanaji wa maji Tanga ni wa kuridhisha

Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online,Korogwe

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo amesema mwenendo wa upatikanaji maji katika Mkoa huo ni wa kuridhisha kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa kuwaondolea adha wananchi ya upatikanaji maji.

Akizungumza na wananchi Kata ya Mtonga, Halmashauri ya Mji Korogwe, Zodo amesema kwa miaka miwili sasa maboresho makubwa yamefanyika kwenye sekta ya maji kwa Serikali kupeleka fedha nyingi kwenye miradi vijijini.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo (wa nne kushoto) akikagua pampu inayovuta maji ardhini. Ni baada ya kufika kwenye Mradi wa Maji wa Kisima Kirefu uliopo Idara ya Maji Korogwe, ambapo mradi huo unasaidia kujaza tenki la Kilole na kusambaza maji kwa wananchi

“Miji ya Korogwe, Handeni na Muheza siku zote ilikuwa na shida ya maji lakini kwa sasa hali ya upatikanaji maji kwa Mkoa wa Tanga inaridhiisha,ukienda kila Wilaya utaona miradi ya maji, na ninyi Korogwe ni mashahidi sasa mnapata maji kwa kiwango cha kuridhisha”amesema Zodo.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa pia mradi wa maji wa miji 28 unakuja ambapo Mkoa wa Tanga umepata miji minne ya Korogwe, Handeni, Pangani na Muheza.

“Hilo sio jambo la kawaida bali ni jitihada za viongozi waobsababu Mkoa wa Tanga tulitakiwa tupate mji mmoja tu hivyo baada ya mradi huo wa miji 28 kukamilika, shida ya maji kwenye miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani itabaki historia,” amesema Zodo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo akishika maji yanayotoka kwenye mradi wa maji wa Kisima Kirefu uliopo Idara ya Maji Korogwe, ambapo mradi huo unasaidia kujaza tenki la Kilole na kusambaza maji kwa wananchi

Awali, Zodo alitembelea mradi wa maji wa kisima kirefu kilichopo Idara ya Maji Korogwe, ambapo akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza, Mhandisi Ulinaula Mwasimba amesema mradi wa maji Mashindei na visima kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Halmashauri ya Mji Korogwe.

Ambao umefanya ongezeko la lita 4,138,000 kwa siku na kufanya jumla ya uzalishaji kwa sasa uwe lita 5,523,000 kwa siku sawa na asilimia 88 ya mahitaji ya lita 6,289,000 kutoka asilimia 32 iliyokuwepo kabla ya kutekelezwa ujenzi wa miradi huo.

Mhandisi Mgaza amesema miundombinu ya utoaji wa huduma ya maji inajumuisha vyanzo, matanki 15 yenye jumla ya mita za ujazo 3,100 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 156.

Mamlaka ya Maji Korogwe ina maunganisho ya wateja wapatao 5,379, wateja wote wamefungiwa dira za maji na upotevu wa maji ni wastani wa asilimia 39 pamoja na kutekeleza uchimbaji wa visima saba katika maeneo ya Majengo, Kwasemangube, Mbeza mawe, Manzese, Mtonga, Mgambo na Kwakombo, ambapo ujenzi wake umekamamilika.

Ujenzi wa mradi wa maji Mashindei hadi hivi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 90 ambapo wamekamilisha ujenzi wa nyumba za pump tatu za Majengo, Manzese na Kwakombo,kulaza mabomba kutoka kwenye visima na kufunga pampu za kusukuma maji kwenda kwenye matenki ya kuhifadhia maji Manzese.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo (wa pili kulia) akipokea taarifa ya upatikanaji maji kwenye Mji wa Korogwe kutoka kwa Mhandisi Ulinaula Mwasimba (kushoto). Ni baada ya kufika kwenye Mradi wa Maji wa Kisima Kirefu uliopo Idara ya Maji Korogwe, ambapo mradi huo unasaidia kujaza tenki la Kilole na kusambaza maji kwa wananchi

Mhandisi Mgaza amesema changamoto iliyopo kwenye Mji wa Korogwe ni
uchakavu wa miundombinu iliyojengwa siku nyingi ambayo haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote hasa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo ya katikati ya mji huo ikiwrmo Mtonga, Masuguru, Manundu Kati, Mbeza, Majengo, Kwamkole, Old Korogwe na Manzese.

Lakini pia, kupasuka kwa mabomba katika maeneo ambayo yalikaa muda mrefu bila kuwa na maji, ukosefu wa miundombinu ya kusafisha na kuchuja maji (Water Treatment Plant), hivyo kufanya maji yanayozalishwa kutokuwa na ubora hasa nyakati za mvua.