Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuunga mkono nguvu za wananchi ili kukamilisha ujenzi wa nyumba ya watumishi Zahanati ya Makanka iliyopo Kijiji cha Masange, Kata ya Gare ili watumishi wapate nyumba ya kuishi karibu na kituo cha kazi.
Nyumba hiyo inajengwa kwa ufadhili wa Mtawa Maria Majelis Urassa (CPS) kutoka shule ya sekondari ya Wasichana Kifungilo iliyopo Kijiji cha Masange kama mchango wake kwa jamii inayowazunguka, huku wananchi wakichangia nguvu zao lakini hadi sasa ni miaka mitano nyumba hiyo haijakamilika huku ikiwa imeshapauliwa.
Mbunge huyo ameeleza hayo baada ya kuitembelea nyumba hiyo Septemba,18 mwaka huu wakati anakagua miradi ya maendeleo kwenye Kata ya Gare, ambapo pia alitembelea shule ya sekondari Masange Juu, nyumba ya mwalimu shule ya msingi Makanka na kituo cha afya Gare.
“Halmashauri mnatakiwa kuunga mkono juhudi za wafadhili na wananchi kwa kumalizia ujenzi wa zahanati hii ya Makanka ambao tayari wameonesha nia ya dhati ya kupata huduma za afya karibu, najua wananchi wameibua miradi mingi nchini sababu mimi nipo kwenye Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, lakini mnatakiwa kuimalizia kwa awamu,”amesema Zodo.
Akisoma taarifa ya zahanati hiyo iliyopo Kitongoji cha Makanka, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Masange Winifrida Kaishiwa
amesema ujenzi wa nyumba hiyo yenye uwezo wa kuishi familia mbili (2 in 1), ulianza mwaka 2018.
Ambapo ukiacha ufadhili wa Mtawa Maria wananchi wamechangia kuchimba kiwanja, kubeba mawe, kupiga tofali, kubeba maji ya kujengea, kutoa mchanga na kubeba mchanga.
“Fedha za Mfuko wa Jimbo awamu ya kwanza mwaka 2020 tulipokea mifuko 50 ya saruji sawa na Tsh.750,000 na tripu mbili za mchanga zenye thamani ya Tsh. 300,000,awamu ya pili mwaka 2022, tulipokea saruji mifuko 100 yenye thamani ya milioni 1.5 ambayo imetumika,” amesema Kaishiwa
Huku gharama ufundi milioni saba hivyo ujenzi ujumla ni milioni 30 ambapo kati ya fedha zilizotumika ni milioni 20 huku akieleza kuwa ili kukamilisha mradi inahitajika kiasi cha milioni 10.
Akiwa shule ya Sekondari Masange Juu, Zodo alisomewa taarifa ya maendeleo na Mkuu wa Shule hiyo Abubakari Kupaza, na kuelezwa kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ni ufadhili wa Mtawa Maria ambapo kati ya vyumba vya madarasa 12 vya shule hiyo11 amejenga yeye kwa kuwezeshwa na Marekani.
Kupaza amesema kwa sasa Mtawa Maria anajenga bweni la wasichana kwa ajili ya kidato cha tano na sita kwenye shule hiyo kwa gharama ya milioni 280 ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 104.
Kwa sasa ujenzi upo hatua ya msingi na gharama zilizotumika ni milioni 43 huku Serikali Kuu kupitia fedha za UVIKO-19, imetoa kiasi milioni 20 za chumba cha darasa milioni 30 za kumalizia maabara.
Kwenye taarifa ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Makanka Yahhi Bombo amesema Mei, mwaka huu shule imepokea kiasi milioni 40 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi nyumba ya mwalimu hadi sasa kiasi cha zaidi ya milioni 29.4, zimetumika, huku fedha zilizobaki benki ni zaidi ya milioni 10.5.
Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Meshack Ikera alimueleza Mbunge kuwa hilo la kukamilisha miradi wamelichukua, na watakamilisha miradi kutokana na bajeti hasa ya Mapato ya Ndani itakavyoruhusu.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024