November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziwa Victoria chanzo cha Maji Shinyanga

Na Penina Malundo, timesmajira

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA),imesema kuwa ziwa victoria imekuwa chanzo kwa wakazi waishio halmashauri ya Shinyanga na miji midogo mitatu katika upatikanaji wa maji ya uhakika.

Akizungumza hayo jana kwa njia ya simu Mkurugenzi Mtendaji,Mhandisi Yusuph Katopola amesema Mamlaka ya Kashwasa inawauzia maji wao na wao kusambaza kwa watumiaji wa maeneo hayo.

Amesema wananchi wanaonufaishwa na maji hayo ni zaidi ya laki mbili wanaoishi katika maeneo ya halmashauri hiyo na miji midogo kama Tinde,Didia na Ipelamagazi.

”Tunapata maji ya ziwa victoria kupitia mamlaka ya maji ya KASHWASA ambapo inatuuzia sisi SHUWASA kisha sisi tunasambaza kwa watumiaji katika halmashauri yetu ya shinyanga na wananchi wanaoishi katika miji midogo mitatu,”amesema na kuongeza

”Hapo mwanzoni huduma ya uhakika ya maji ilikuwa ngumu kupatikana na hata kufanya shughuli za kijamii ilikuwa ni changamoto ila tangu maji haya yalipoanza kutoka ziwa victoria kutufikia shinyanga mambo yamekuwa mazuri mno,”amesema.

Mhandisi Katopola amesema mikakati waliyonayo kama SHUWASA ni kuhakikisha maji hayo ya ziwa victoria yanawafikia watu wengi zaidie ambapo serikali kupitia Wizara ya maji imefanikiwa kupata kiasi cha sh. Bilioni 195 kwaajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi ,usafi wa mazingira na kuijengea uwezo taasisi ya yao.

Amesema mkakati huo unalengo la kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika masaa 24 na kuwa endelevu kwa wakazi hao.”Changamoto ambayo tunakabiliana nayo ni mtandao wa maji kutotosheleza watumiaji wote,endeo la manispaa na miji midogo yake hayana miundombinu ya uondoaji wa maji taka pamoja na uelewa mdogo wa wananchi katika kulipia huduma ya maji kwa hiari mpaka mamlaka iwakatie maji,”amesema.

Kwa upande wake Elizabeth Bugehu (75) Mkazi wa Kitangiri Manispaa ya Shinyanga amesema huduma ya maji kwa sasa katika mkoa wao imeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto walizokuwa wanakumbana nazo kipindi cha mwanzoni.

Ameishukuru SHUWASA chini ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha inawajali wananchi wake na kuendeleza dhamira zake za kuhakikisha inamtua mama maji kichwani kwa kuwafikishia wananchi maji kwa urahisi zaidi kutoka ziwa victoria.

”Nilipoona kwa mara ya kwanza napata maji ya bomba kutoka ziwa victoria nilifurahi sana sana kwani mwanzo tuliangaika sana katika kupata maji ilifika kipindi tunawahi foleni alfajiri,”amesema.