January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafuasi wa ACT Wazalendo wakiwa kwenye mkutano wa kampeni

Zitto ayapa kipaumbele mambo manne Kigoma Mjini

Na Mwajabu Kigaza , Kigoma

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama Cha ACT wazalendo, Zitto Kabwe amesema iwapo akichaguliwa kuwa mbunge atafanyia kazi mambo manne kati ya 11 ambayo tayari yameshafanyiwa kazi, ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni zake wakati anaomba ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2015.

Zitto alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za ACT Wazalendo katika Jimbo la Kigoma Mjini ambapo uzinduzi huo ulifanyika eneo la Kawawa, Manispaa ya Kigoma Ujiji .

Zitto alisema ahadi 15 alizozitoa mwaka 2015 kati ya hizo 11 zimekamilika, zikihusisha ujenzi wa barabra za ndani ya Manispaa ya Kigoma Ujiji yenye urefu wa kilometa 15 pamoja na ujenzi wa forodha ya Ujiji.

Pia aligusia ahadi nne ambazo hazijakamilika na kuomba kuongezewa muda ili aweze kuzikamilisha ahadi zilizobaki .

“Endpo mtanipa ridhaa ya kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano naahidi kutekeleza mambo manne yaliyobaki na lengo langu ni kuipandisha Kigoma katika hadhi inayohitajika na baada ya miaka mitano kwisha mnaweza kufanya maamuzi nani mtamuweka katika nafasi hii ya ubunge,” alisema Zitto.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao walihudhiria ufunguzi wa kampeni hizo akiwemo Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo na mgombea udiwani kata ya Bangwe, Hussen Ruhava.

Wanasiasa hao vijana walisema vijana wanahitaji ajira na sasa mkoa wa Kigoma kuna chuo cha uzalishaji wa mbegu za mchikichi na hilo limefanikiwa mara baada ya Zitto kulipigia kelele, hivyo ipo haja ya kuendelea kumchagua ili aweze kuendelea kufanya mabadiliko katika mkoa wa Kigoma hususani Jimbo la Kigoma mjini.