Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuhakikisha wanafanyakazi kwa kutoa huduma kwa wakati ili kuwa na ufanisi na tija ionekane kwa wananchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Uzinduzi wa Kituo Kikuu cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dar es salaam kilichogharimu shilingi bilioni 4.09 kilichopo Wilaya ya Temeke leo tarehe 28 Aprili 2023. Amesema baadhi ya changamoto ya uchelewaji wa Jeshi la zimamoto na uokoaji katika kufika eneo la tukio ni ujenzi holela pamoja na vituo vya jeshi hilo kuwa mbali na makazi ya wananchi hivyo ameiasa Wizara ya Ardhi na mamlaka zinazohusika kuendelea kudhibiti ujenzi holela ili kuhakikisha maeneo ya makazi yanakuwa na barabara za kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wa dharura.
Dkt. Mpango amesema katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano ni vema Jeshi hilo kujipima ni kwa kiasi gani limefanikiwa katika utoaji huduma ya zimamoto na uokoaji nchini. Amesema ni lazima kuhakikisha mfumo wa kiutendaji wa jeshi hilo una tija katika utoaji huduma kwa jamii. Ameongeza kwamba ni lazima kuhakikisha wanakua imara na tayari kukabiliana na majanga ya moto na majanga ya aina nyingine kama matetemeko ya ardhi, mafuriko, vimbunga na ajali kama zile za barabarani, anga na majini kwa haraka katika wakati huu wa ongezeko la watu na ukuaji wa miji nchini.
Pia Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga zaidi vituo vya zimamoto na uokoaji. Ameongeza kwamba kwa upande wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya zimamoto na uokoaji katika Wilaya zote nchini ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati na kuzuia athari zaidi.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufanyia kazi eneo la ukaguzi wa kinga na tahadhari ikiwemo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kusoma ramani za majengo na kutoa ushauri, hususan katika maeneo ya makazi ya binadamu. Ametoa rai kwa jeshi hilo kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa na ukaguzi husika unafanyika kabla ya ujenzi wa vituo vya mafuta vinavyojengwa karibu na makazi ya binadamu ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kujielekeza katika kuweka mifumo ya TEHAMA ambayo itawezesha kutoa huduma za kimtandao katika ofisi za zimamoto ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi na kuwezesha utoaji wa huduma kwa haraka.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa kituo hicho, Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji John Masunga amesema jitihada za kusogeza huduma za zimamoto na uokoaji kwa wananchi zinaendelea ambapo jeshi hilo kwa linatarajia kujenga vituo katika mikoa saba ya Manyara, Geita, Simiyu, Njombe, Katavi, Songwe na Kagera. Kamishna Masunga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa shilingi bilioni 10.5 tangu kuingia madarakani katika kuimarisha huduma za jeshi hilo.
Amesema Jeshi hilo linaendelea kuboresha makazi ya maafisa na askari ambapo tayari serikali imetoa shilingi bilioni 3.3 kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo sita kati ya nane ya ghorofa yanayojengwa katika eneo la kikombo jijini Dodoma. Ameongeza kwamba jumla ya askari 479 wameajirwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita pamoja na kupandisha vyeo maafisa na askari 1118 na kutoa mafunzo kwa askari na maafisa 1168.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best