December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zidane: Sergio Ramos kurejea mkondo wa pili dhidi ya Chelsea

MADRID, Uhispania

KOCHA mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane amesema, ana matumaini kuwa nahodha wake mwenye ushawishi mkubwa katika klabu hiyo Sergio Ramos, anaweza kurejea dimbani katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo.

Ramos, mwenye umri wa miaka 35 raia wa Uhispania, amecheza mara tatu tu kwenye mashindano yote tangu mwanzoni mwa mwaka na alikosa ushindi wa robo fainali dhidi ya Liverpool, pia kwenye mchezo wa sare ya goli 1-1 mkondo wa kwanza dhidi ya Chelsea huko Valdebebas Jumanne usiku, lakini kuna nafasi anaweza kurejea kwenye mechi ijayo ya mkondo wa pili kutokana na afya yake kuimarika.

“Natumai atakuwa pamoja nasi, lakini sijui sasa hivi. Sergio bado hajafanya mazoezi na timu hiyo, kwa hivyo tunasubiri kuona ikiwa anajiunga nasi. Natumai anaweza kurejea haraka iwezekanavyo, ”Zidane amesema juu ya hali hiyo, kupitia RealMadrid.com.

Real pia hawakuwa na beki wao wa kushoto Ferland Mendy na kiungo mkabaji Fede Valverde katika mchezo wa juzi, lakini kocha Zidane ana matumaini pia kurejea kwa wakati wachezaji hao wiki ijayo Stamford Bridge.

Bao la ugenini la Chelsea linaiweka Real katika wakati mgumu kwenye mechi ya mkondo wa pili huko London, lakini Zidane alifurahishwa na jinsi timu yake ilivyomudu katika mazingira magumu na anajua vizuri kwamba lazima wacheze kadri ya uwezo wao kuhakikisha wanapata bao katika mchezo ujao.