January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Waziri Mwambe yaleta nuru Masasi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar Mtwara

ZIARA ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini Mkoani Mtwara, Geoffrey Mwambe imeacha alama kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo mara baada ya kufanikisha kufanya maboresho kadhaa yenye kuleta nuru kwa maendeleo jimboni humo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Kata ya Matawale iliyopo jimboni hapa na kukabidhi mabati 200 kwa ushirikiano na Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Gereza la Wilaya ya Masasi, Waziri Mwambe amesema serikali imedhamiria kuleta maendeleo na kutatua changamato zinazowakabiri na kuwataka wakazi hao kuwa na imani ya serikali yao.

“Ninakabidhi mabati haya kwa ushirikiano na wenzetu wa TPB, lakini nataka niwaambie kuwa Serikali ipo pamoja nanyi na ina malengo mazuri kuhakikisha tunafikia maendeleo na kuondoa changamoto hivyo niwaombe muwe na imani na Serikali iliyo chini ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan,”amesema.

Amesema Serikali kwa kuona umuhimu wa afya kwa wakazi wa maeneo hayo, imeamua kuwapati fedha takribani milioni 500 kwa ajili ya ukarabati mkubwa na upatikanaji wa dawa katika hospitali ya Mkomaindo iliyopo jimboni hapa.

“Kilio chetu cha kuboreshewa kituo chetu cha afya na upatikanaji wa dawa kimesikika na Serikali imetutengea milioni 500 kwa ajili ya hospitali ya Mkomaindo”

Kwa upande wa elimu, Mwambe mbali ya kuchangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi darasa alisema Serikali imewapatia fedha milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule sekondari ya matawale.

“Ninafahamu kuwa kuna changamoto ya uhaba wa madarasa, lakini ninakabidhi hii mifuko 50 ya saruji kubwa zaidi nataka mjue kuwa kwenye kata hii ya Matawale tumepewa milioni 400 kwa ajili ya kujenga shule ya sekondari hapa,” alisema Mwambe.

Ameongeza kuwa kwa kuona umuhimu wa miundombinu Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwapatia fedha bilioni 1.5 kwa ajili ya kuweka rami barabara za Masasi mjiji huku pia milioni 700 zikitumika kwenye ukarabati njia zinazounganisha jimbo hilo na majimbo mengine.

Aidha Mbunge huyo amewaomba wananchi hao kuwa wavumilivu kwenye suala la maji kwa kuwa tayari amehakikishiwa na idara ya maji RUWASA kuwa ndani ya mwaka huu kitajengwa kisima kirefu kitakachowasaidia kupata maji ya kutosha na kupunguza kero ya maji.

Kwa upande wake, Hamisi Mnela ambaye ni Diwani kwenye kata ya Matawale amemuhakikishia Mbunge huyo kuwa wananchi wako tayari kushirikiana nae kuhakikisha maendeleo yanafikiwa jimboni hapo.

“Mimi nataka nikuhakikishie mbunge wetu kuwa sisi tuko pamoja na wewe na tunatambua na kuthamini jitihada zako za kuleta maendeleo kwetu hivyo na sisi hatutokuangusha na Mungu akusimamie kukamilisha mazuri uliyonayo kwetu”, amesema Mnela.