Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mgombea wa Urais wa CCM,Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokelewa kwa shangwe kubwa Tukuyu Mjini. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye
ameambatana wa viongozi mbalimbali wa kitaifa wa CCM akiwemo Katibu Mkuu Dkt. Asha-Rose Migoro na Katibu wa itikadi na uenezi Kenan
Kihongosi na viongozi wengine wa chama wa mkoa na wilaya.
Dkt. Samia alisisitiza kuwa dhamira ya CCM ni kuhakikisha kila kijiji na kila kitongoji kinapata huduma bora za msingi. Kama kuna shida ya maji, miradi ya maji italetwa.
Kama kuna changamoto ya umeme, vijiji
vimeshaunganishwa na sasa huduma inasogea katika kila kitongoji ili kila kaya
ipate umeme.
Aidha, shule na vituo vya afya vinaendelea kujengwa vijijini kwa
ubora wa hali ya juu ili wananchi wapate huduma karibu.
Akizungumzia sekta ya kilimo na mazao ya biashara, Dkt. Samia alitumia muda
kueleza kuhusu zao la chai na parachichi. Kuhusu chai, anaeleza kuwa mashamba yaliyokabidhiwa kwa wawekezaji binafsi kama WATCO na
MOHAMED ENTERPRISES yalitolewa kwa imani kuwa yataendeleza sekta hiyo.

Anasema serikali iliweka mazingira rafiki ya uwekezaji, ikiwemo sera, sheria na
miundombinu ya maji na umeme. Hata hivyo, changamoto zimejitokeza, na
hivyo serikali imeunda timu maalumu ya kufanya tathmini ya mashamba na
viwanda vya chai,lengo ni kuhakikisha mashamba hayo yanamilikishwa kwa
vyama vya ushirika chini ya uongozi wa serikali, ili kuongeza thamani ya chai
kabla ya kusafirishwa.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali imetoa maelekezo kwa wawekezaji waliopo
kulipa madeni yao kwa wakulima na wafanyakazi wa viwanda, kabla serikali
haijachukua hatua ya kuhamisha umiliki. Aliwaahidi wananchi wa Rungwe
kwamba madeni hayo yatalipwa katika kipindi kifupi atakapochaguliwa tena
kuliongoza taifa letu.

Kuhusu zao la parachichi, Dkt. Samia amefafanua kuwa zao hilo sasa lina soko
kubwa duniani, na Tanzania inashika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha
parachichi bora. Changamoto inayokumba sekta hii ni kushuka kwa bei,
jambo linalowavunja moyo wawekezaji. Hata hivyo, serikali ya CCM
imepanga kujenga vituo 50 vya kuhifadhi parachichi na mbogamboga, viwili
kati ya hivyo vitajengwa Rungwe. Vituo hivyo vitasaidia kuhifadhi mazao kwa
miezi mitatu, ili wakulima wasiuze kwa bei ya hasara, bali wasubiri soko liwe juu.
Katika hatua nyingine Dkt Samia amesema , kupitia mpango wa kongani za
viwanda na programu ya BBT, serikali atakayoiunda itawekeza kwenye
viwanda vya vijana vitakavyoongeza thamani ya parachichi. Parachichi
ambazo zitaharibika zitatumika kutengeneza bidhaa nyingine kama mafuta
ya parachichi, chakula cha mifugo na bidhaa mbalimbali za viwandani. Ili
kuendeleza zao hili, serikali imeamua kuwaajiri maafisa ugani
watakaowasaidia kupima afya ya udongo na kuwapatia maarifa bora ya
kilimo, pamoja na kutoa pembejeo na huduma za ugani.

Dkt. Samia amesisitiza
kuwa ruzuku ya serikali itaendelea, ikiwemo mbolea na dawa za kupulizia, ili
kuongeza tija na kuhakikisha zao la parachichi linakuwa nguzo ya uchumi wa
wananchi wa Rungwe.
AKIWA MBARALI
Kwenye mkutano wake wa pili Mbarali, Mgombea wa Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwashukuru wananchi wa Mbarali kwa mapokezi
makubwa na imani yao kwa CCM na kusisitiza kwamba Mkoa wa Mbeya
umewaka kijani.
Amewapongeza viongozi wa CCM kwa kazi kubwa waliyofanya
na kuwakumbusha wananchi kwamba miaka mitano iliyopita, serikali ya CCM
imetekeleza mikakati mingi ya kimaendeleo katika sekta zote muhimu.
Kuhusu sekta ya afya, wilaya ya mbarali, alibainisha kwamba hospitali moja
ya wilaya imejengwa, vituo vya afya vinne na zahanati tisa zimeongezwa.
Vifaa tiba na watumishi wamepelekwa, na sasa wananchi wanapata vipimo
na huduma muhimu kwenye hospitali ya wilaya. Kwenye elimu, shule mpya za
msingi 35 na sekondari 14 zimejengwa, sambamba na kuongeza walimu na
madarasa kwenye shule zilizopo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Kwa upande wa maji, serikali imetenga shilingi bilioni 10 kupitia RUWASA kwa
ajili ya visima 30. Aidha, miradi 11 ya maji kutoka vyanzo vya mito na matanki
mawili ya kuvuna maji ya mvua imetekelezwa. Zaidi ya shilingi bilioni 51.5
zimeelekezwa kwenye mradi mkubwa wa maji wa miji 28, ambao
utawafaidisha wananchi wengi wa Mbarali kupata maji safi na salama.
Dkt. Samia amekumbusha kuwa baada ya kuhakikisha vijiji vyote vya wilaya ya
Mbarali vimeunganishwa na umeme, sasa serikali inaendelea kumalizia
vitongoji. Kati ya vitongoji 712, tayari 641 vimeunganishwa na huduma hiyo, na
ameahidi kumalizia vilivyosalia ili kila kaya ifikie maendeleo.
Sekta ya miundombinu pia imepewa kipaumbele, ambapo zaidi ya shilingi
bilioni 11 zimetumika kujenga barabara za lami kupitia TARURA, pamoja na
madaraja manne. Zaidi ya kilomita 464.5 za barabara za changarawe
zimeboreshwa ili kuhakikisha zinapitika mwaka mzima.
Aidha, ameeleza
umuhimu wa kuhamisha vijiji vitano vilivyokuwa ndani ya Hifadhi ya Ruaha,
kwani hifadhi hiyo ndiyo chanzo cha maji kinachozalisha umeme Mtera na
Kidatu.
Amesisitiza kuwa bila kulinda hifadhi hiyo, taifa lingekabiliwa na upungufu
mkubwa wa umeme.
Kuhusu fidia, amewahakikishia wananchi kwamba tathmini ya madai ya fidia
kwa walioathirika itakamilishwa ili wote walipwe. Aliongeza kuwa serikali
imeamua kununua shamba la uwekezaji la Mbarali Estate kwa ajili ya kuligawa
kwa wananchi, kutokana na changamoto ya ufinyu wa mashamba.
Akitoa mwelekeo wa awamu inayofuata, Dkt. Samia aliahidi kukamilisha
miradi yote ya maji safi na salama, kujenga barabara za mitaa kwa kiwango
cha lami, ikiwemo barabara ya Kagomba–Ukaguzi na Utego kuelekea
viwandani.
Aidha, mtandao wa barabara za lami utaendelezwa katika
maeneo ya Igava, Lujewa, Ubaruku, Chimala, Igurusi, Majimbila na Kapunga,
kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora za kisasa.
Kwa dhamira ya kujenga Tanzania inayojitegemea, alisisitiza kuwa kila mradi
utakaoanzishwa Mbarali utamalizika kwa wakati na kwa ubora, na wakati huo
huo miradi mipya itaendelea kuanzishwa na kukamilishwa.
Aidha, amesema
serikali itaimarisha mifumo yake ya utendaji ili wananchi wa Mbarali waweze
kufanya kazi zao kwa bidii, weledi na mafanikio, bila vikwazo vya huduma za
msingi.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina