December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Meya Ilala yaibua madudu Buguruni

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MEYA wa Halmashauri ya Ilala Omary Kumbilamoto katika ziara yake ya kutembelea wilaya hiyo kukagua miundombinu ya barabara imeibua madudu kufuatia mkandarasi wa ujenzi Barabara ya Mnyamani kushindwa kufika eneo la kazi wakati akiwa ameshalipwa sh.mil.70

Katika ziara hiyo aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Meya wa Ilala Saddy Kimji,diwani wa Kata ya Mnyamani Shukuru Dege,viongozi wa TARURA pamoja na mhandisi wa manispa hiyo John Magori.

Kumbilamoto amesema madhumuni ya ziara hiyo ni kufuatilia miradi ya maendeleo iliyopo katika Manispaa ya Ilala na fedha zinavyotumika ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati kulingana na fedha zilizotengwa.

Mhandisi wa Manispaa ya Ilala John Magori akimashika mkono Meya wa Ilala Omary Kumbilamoto wakati wa ziara ya kero kata ya Tabata jana eneo la Bonde la Msimbazi katika mradi wa mifereji inayojengwa na mradi wa kuboresha miundombinu. Mpigapicha Wetu

“Nikiwa kama Meya wa Manispaa ya Ilala ni lazima nifuatilie matumizi ya pesa za Serikali zinazotolewa n Rais John Magufuli ili kuhakikisha kuwa kasi aliyonayo inaendana na manispaa yetu katika utekelezaji wa ilani”amesema Kumbilamoto.

Kumbilamoto amesema kuwa ameshangazwa na kitendo cha mkandarasi huyo kuacha kukamilisha ujenzi wa kipande cha barabara cha Buguruni Mnyamani kwenda Hospitali ya Plan wakati akiwa tayari amelipwa fedha za mradi huo.

Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu (katikati) akizungumza na Meya wa Ilala Omary Kumbilamoto pamoja na Naibu Meya Wa Ilala Saddy Kimji na Maafisa wa TARURA wakati ziara ya kutatua kero Wilaya ya Ilala.Picha na Heri Shaaban

“Nimeshangazwa na kitendo cha mkandarasi wa Kampuni ya BECO LTD alisaini ujenzi wa barabara hiyo kwa gharama ya sh.mil.130 ambapo kati ya fedha hizo tayari amelipwa sh.mil.70 lakini hadi sasa ni mwezi mmoja bado hajafika eneo la ujenzi ili kuanza kazi jambo linamshangaza,” amesema.

Kutokana na kitendo hivcho meya Kumbilamoto alitoa agizo kwa Meneja wa TARURA wilaya kumwandikia barua ya onyo mkandarasi huyo, pamoja na kumwita mkandarasi huyo amsimamie ujenzi na uishe kwa wakati.

Amesema anampongeza Rais John Magufuli katika utekelezaji wa Ilani sambamba na kusimamia miradi yake ya maendeleo ambayo imeelekezwa Halmashauri ya Ilala.

“Katika halmashauri ya Ilala tunafanya vizuri kila mwaka tunapata hati safi kuanzia 2015/2016 2016/2017,2018/2019, 2019/2020 hivyo lazima tujiridhishe na miradi yetu ya maendeleo ” amesema.

Meya wa Halmashauri ya Ilala Omary kumbilamoto (katikati)akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa barabara ya Mnyamani Dar salaam jana (kulia wa pili) Naibu Meya wa Ilala Saady Kimji .

Kwa upande wake Naibu Meya wa Manispaa ya ILALA Saady Kimji amesema ziara hiyo ni ya kutatua kero na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM.

Naibu Kimji ameema wakati sasa umefika lazima tuwatumikie wananchi wetu,sisi kama viongozi wa halmashauri amna kulala ziara hizi ni endelevu.

Kimji amempongeza Rais John Magufuli kwa kuwapatia miradi mikubwa Ilala ikiwemo miradi mkakati wataisimamia na kuitunza ili uchumi uweze kukua Wilaya Ilala.

Katika ziara hiyo ametembelea Jimbo La Ilala, Jimbo la Segerea na Jimbo la Ukonga ikiwemo pia kuangalia miradi inayosimamiwa na Benki ya Dunia.