November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Dkt.Samia ilivyoiimarisha kiutendaji Katavi

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline

“IPO mifumo ya kufuatilia rushwa wakati wa uchaguzi mgombea yeyote atakayetoa, Jina lake litakatwa” Hii ni kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta mara baada ya kutamatika ziara ya kikazi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani humo.

Kauli hiyo imeibua minong’ono ya sitofahamu, Wapo wanaohoji itawezekana kwa namna gani? Na wapo wanaosema kuwa haitawezekana kwani wapiga kura wenyewe kwa sasa ni wenye kuomba rushwa.

Lakini hilo halizuii mtazamo wa namna ziara ya Rais Dkt. Samia ilivyoleta sura tofauti ya utendaji kazi kwa viongozi wa CCM na serikali jinsi ambavyo maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa yanavyotegemea sanduku la kupigia kura.

Siku nne za ziara hiyo ya kikazi Rais Dkt. Samia aliyofanya Julai 12 hadi 15, 2024 akikagua ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege Mpanda uliogharimu Bil 1.4.

Ukaguzi wa uingizwaji wa umeme wa gridi ya taifa unaohusisha ujenzi wa vituo vya kupokea,kupozea na kusambaza umeme uliogharimu Bil 48 na ujenzi wa njia ya umeme Bil 106.

Vilevile akifungua jengo lenye thamani ya Bilioni 1.4 la Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi,Ukaguzi wa vihenge vya Taasisi ya taifa ya uhifadhi wa mazao ya chakula (NRFA) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

Ziara hiyo ikihitimishwa kwa hotuba ya hadhara wakati akifunga wiki ya wazazi kitaifa katika viwanja vya CCM Azimio Manispaa ya Mpanda,Ni wazi ulifungua milango ya kuimarishwa kwa CCM Mkoa wa Katavi kisiasa na viongozi wa serikali kufuata misingi ya utawala bora.

“Tumepata maelekezo ya kiuongozi kwa ajili ya mstakabali wa taifa letu” amesema Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta.

Kimanta anaeleza kuwa hawawezi kukubali kudhoofisha utawala bora na demokrasia kutokana na wagombea kutoa rushwa kwani kufanya hivyo ni kudhalilisha utu wa mpiga kura kwamba hana maana yeyote kwenye uchaguzi.

Anasema wakipata viongozi kwa njia ya rushwa wataitesa jamii kwa sababu hawataona kwamba dhamana waliyopata haitokani na wananchi bali inatokana na fedha zao walizotoa.

“Ni kweli tumezungumza na viongozi wakuu wa kitaifa, Rushwa katika uchaguzi ni changamoto unaweza kukuta rushwa inaharibu mfumo wa uongozi nanyi mmekuwa mashahidi mtu anachaguliwa baada ya muda fulani kupita wananchi hawamtaki tena…sasa unashangaa ni nyie mlimchagua lakini tena mnamkataa,”anasema Kimata.

Anaongeza “Jambo moja ambalo sitaki kuliamini la kuwa mbunge nila watu wenye fedha,Mimi kama Mwenyekiti nachoweza kusema ni hapana sio la watu wenye fedhaa la msingi ni kubadilisha mtazamo wa kifikra na kutambua yeyote anaweza kuwa mbunge”

“Changamoto tunayoipata ni nini jamii yetu inavyolitizama suala la rushwa wako tayari kupewa kipande cha nguo tu na wakasema huyo ndiye anayetufaa na bila kujua wataharibu mfumo kwa muda wa miaka 5 na tatizo hilo liko kwa wananchi,”anasema.

Anabainisha kuwa tunapoelekea uchanguzi jamii inapaswa kuikataa rushwa “ Anayetoa na kupokea rushwa wote wanamakosa anayetaka kupata uongozi kwa kutoa rushwa hatufai na dawa ya rushwa ni kutengeneza jamii inayokataa rushwa”

Wasiwasi mkubwa ni namna gani vitendo vya rushwa vitadhibitiwa, Kimata amesema ni muhimu kwa wananchi na taasisi mbalimbali kushirikiana katika kupambana na rushwa ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Katika kutoa minong’ono na maswali mengi Kimata anasema chama kimejipanga kufuatalia mienendo yote ya wagombea watakao jitokeza.

“Nitoe angaliizo kwa wagombea huko mbele ya safari tusije tukalaumiana nawaambia kabisa wagombea watakao dhani kwamba Katavi ili wawe viongozi watatumia fedha wajiandae kisaikolojia”anasema.

Anafafanua kuwa wanahitahi kupata viongozi ndani ya mkoa wa Katavi ambao wananchi wanawataka kwa kuwatumikia na kwa kukijenga chama na sio kwa kujijenga yeye mwenyewe binafsi.

“Mtaona chama kwanza mtu baadaye maana kunadesturi maeneo mengine lakini unasikia wapiga kura wangu wako benki.Ni kweli unaweza kuwatoa benki lakini wasifike kwenye vikao vya uteuzi hawatashiriki pesa inakwenda na kwenye uteuzi haupo”anasisitiza Kimanta.

Anaweka wazi kuwa kila mgombea atakaye kuja kugombea mkoani humo ataambiwa kwani katika chama adui mkubwa ni rushwa na kuna miongozo na maelekezo ambayo yatafuatwa na sio mahusiano ya kufahamiana.

Katika hatua nyingine anasema licha ya ziara ya Rais Dkt.Samia kuwa jenga kiuongozi kwenye kusimamia masuala mbalimbali ya kiutendaji pia ziara hiyo imeupima uwezo wa mkoa katika huwadumia wageni wengi zaidi katika maeneo ya chakula na malazi ambapo amebaini uwezo huo umefanikiwa.

Waziri Mkuu Msitaafu, Mizengo Pinda akizungumza na mtandao huu Julai 19, 2024 nyumbani kwake katika kijiji cha Kibaoni,Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameungana na mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo kwamba rushwa inapaswa kukemewa.

Wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025,anakemea wanasiasa wanaotumia fedha ili kuwashawishi wananchi wawachague.

Pinda anasema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, kuna baadhi ya watu wanaotaka nafasi kwenye ngazi mbalimbali hutumia fedha kuwashawishi wananchi kwa kuwapatia rushwa.

Anasema jambo hilo halipaswa kuachwa litamalaki, bali likemewe kwa nguvu zote kwa kuwa halistahili katika kupata kiongozi bora.

“Serikali imeweka utaratibu na bahati nzuri Serikali iliyopo madarakani inaongozwa na chama tawala na inasimamiwa na ilani ya uchaguzi, pia, kuna Katiba na kanuni na vitu vingine, vinaelekeza vizuri vitu vya kufanya na ambavyo si vya kufanya kwenye uchaguzi,”amesema Pinda.

“Vikwazo vipo kwenye matumizi ya fedha (rushwa) kwenye uchaguzi, ukiangalia kuna watu kwenye macho ya wengi hawastahili kuwa na cheo chochote serikalini, lakini ana vifedha ikifika kwenye uchaguzi, anaomba nafasi na siku ya kuamkia uchaguzi, yeye halali usiku, anaandaa watu wake ambao wanatembea nyumba kwa nyumba kuzungumza na wananchi na kuwaachia kitu kidogo ili kuwashawishi wamchangue.

Anasisitiza “Hii inahitaji very strong mind kwa wananchi kusema ‘pamoja na kahela ulionipa sikuchagui, namchagua mtu ninayemtaka mimi’. Binafsi natamani kuwa na watu wengi wa namna hiyo, kwamba kula hela yake na anamchagua mtu anayefaa kuwa kiongozi na sio bora kiongozi”

Mkazi wa Kijiji cha Mwamkuru Manispaa ya Mpanda mkoani humo, Martha Jordan amempongeza Rais Dk Samia kwa kazi nzuri ya maendeleo anayoifanya.

Martha anasema wanashuhudia maendeleo makubwa kwenye sekta za kilimo ambapo katika kijiji cha Mwamkuru zaidi ya fedha Bilioni 31.6 zinatumika ujenzi wa sikimu ya umwagiliaji.

Anasema sio kwenye sekta ya kilimo pekee bali iwe afya,maji,elimu,barabara,usafiri wa anga na reli kote huko kazi kubwa imefanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.