Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Zanzibar
Waziri wa Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zanzibar Riziki Pemba Juma amesema wizara hiyo inatarajia kutoa vitambulisho 25,000 vya wazee wote wanaopokea pencheni jamii ili viweze kutumika katika huduma mbali mbali ikiwemo wakati wa kupokea pencheni jamii.
Kauli hiyo ameitoa nwishoni mwa wiki wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maoni, ushauri/mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwaka wa fedha 2022/2023, huko Chukwani, Unguja.
Amesema Jumla ya vitambulisho 25,000 vinatarajia kupatikana kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambavyo watapewa wazee wote wanaopokea pencheni jamii.
Amesema Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumza za SMZ wanaendelea na utaratibu wa kuwatengenezea vitambulisho hivyo.
Hata hivyo Waziri huyo amesema jumla ya vitambulisho 3,668 tayari vimeshatolewa kati ya walengwa 28,776 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.
Aidha amesema Wizara hiyo imetoa mafunzo ya utoaji wa huduma za mpango wa pencheni jamii kwa masheha wapya 31 wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja na masheha 30 wa Wilaya ya Wete na Micheweni, Pemba ikiwa ni juhudi za kuwajengea uwezo katika utoaji wa huduma za pencheni jamii.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa Wizara hiyo inatumia njia mbalimbali kuelimisha jamii juuya pencheni jamii kwa kutumia mitandao ya kijamii ikiwemo, facebook, twitter, Instagram na Youtube pamoja na kushiriki katika matamasha ya maonesho mbali mbali.
Wakati huo huo amesema Wizara hiyo imekamilisha uhakiki wenye lengo la kujiridhisha uwepo wa wazee ambapo jumla ya wazee 11,850 huku kati yao kwa upande wa Unguja wazee 4,388 ni wanufaika wa mpango wa pencheni jamii.
“Uhakiki huo ulifanyika nyumba kwa nyumba kwa upande wa Unguja katika Wilaya zote na Pemba kwa wilaya ya Mkoani, Wete na Micheweni,, hivyo tumejiridhisha uwepo wa wazee wanaonufaika na mpango wa pencheni jamii’,”amesema Waziri Pembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwaka wa fedha 2022/2023, Sabiha Filfil Thani amesema kamati hiyo inapongeza Wizara hiyo kwa kuweza kukamilisha zoezi la uhakiki wa wazee wanaonufaika na pencheni jamii pamoja utengenezaji wa vitambulisho.
“Katika kukuza hadhi na majukumu ya Idara ya Ustawi wa jamii na Jinsia kamati ilishauri Wizara kuharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya wazee waliyofikia umri,tunashukuru kwa kupokea ushauri huo na kuufanyika kazi na kuanza kuwapatia wazee vitambulisho hivyo,” amesema Thani.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja