Na Angela Mazula TimesMajira Online
WASINDIKAJI wa mchele mkoani Morogoro wameahidiwa fursa za kuuza mchele kwa wafanyabiashara kutoka Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku ya wasindikaji kutoka wilaya tano za Mkoa wa Morogoro wilayani Ifakara wiki hii, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare amesema amefanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah.
“Nilimuomba Makamu wa Pili wa Zanzibar awashauri wafanyabiashara kuacha kuagiza mchele kutoka nchi za Asia na badala yake waje huku Morogoro kununua bidhaa hii,” amesema Sanare.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Mchele nchini, Winnie Bashagi amesema Mkoa wa Morogoro ulizalisha tani 800,000 kwa msimu uliopita, kati ya hizo, tani 400,000
zilitoka katika Wilaya ya Ifakara.
“Jumla ya tani milioni 2.8 zilipatikana wakati wa msimu uliopita na kuwa na ziada ya tani milioni 1.2 na katika msimu huu tunakadiria tani za ziada milioni 1.8”, amwsema Winnie
Bashagi.
Hata hivyo, Bashagi amesema kwamba kwa sasa kila kaya inakadiriwa kutumia wastani wa kilo 25 za mchele, tofauti na miaka ya nyumba ambapo mchele ulikuwa unanunuliwa wakati wa sikukuu tu.
Mkuu wa Wilaya ya Ifakara, Ismail Mlawa amesikitishwa na baadhi ya wasindikaji kutoka wilayani kutohudhuria warsha hiyo muhimu kwa kisingizio kwamba walikuwa wanasimamia biashara zao.
“Niwaombe mliofika hapa kwamba mkatoe elimu kwa wenzenu ambao wameshindwa kufika ili tuendelee kupata mchele ulio bora zaidi”, amesema.
Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kwamba wasindikaji wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuchangia katika mapato yatokanayo na kodi.
Wasindikaji hao waliiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu, hasa Barabara za Vijijini pamoja na kutatua tatizo la kukatika kwa Umeme.
Mwasiti Mbombe Mkulima kutoka Turiani wilaya ya Mvomero amesema umeme unakatika bila kupewa taarifa na hivyo hurudisha nyuma shughuli za usindikaji.
“Kutokana na kukatika kwa umeme, tena bila hata kutoa taarifa, tunawapoteza wateja wengi pia kuzorotesha ukuaji wa kipato kwa wafanyabiashara”, amesema.
Akizungumza katika warsha hiyo, Mtalaam wa Mawasiliano Mwandamizi kutoka REPOA, Godfrey Kalagho amesema mafunzo hayo ni sehemu ya programmu ya utafiti na kujenga uwezo wa watunga sera, wazalishaji, na wauzaji biadhaa nje ya nchi kutathimi sera na kusaidia kuboresha ushindani na kutanua wigo wa masoko.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na Jumuia ya Ulaya na kusimamiwa na Sekretiati ya Jumuiya ya nchi za Africa, Caribbean, na Pacific (OACPS), na kutekelezwa na REPOA na taasisi ya mafunzo ya maendeleo ya Chuo Kikuu cha Erasmus Rotterdam (ISS).
Maeneo mahususi ya mradi huo ni bidhaa za mboga mboga, mchele, ngozi, mwani na huduma za usafirishaji.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo