April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zanzibar Insuarance watoa msaada wa Pads kwa wanafunzi sekondari ya Macechu Tanga

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

WANAFUNZI wa kike zaidi ya 600 wa shule ya sekondari Macechu iliyopo jijini Tanga wamelalamikia uhaba wa vyoo vya wasichana jambo ambalo limekuwa likisababisha adha kwao wakati wanapokwenda kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi huku baadhi yao wakikosa masomo kwa kubaki majumbani kwa kuhofia usalama wao.

Wakizungumza wakati walipokuwa wakipokea taulo za kike shuleni hapo wanafunzi hao wameomba msaada wa vyoo kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Scolastika Mtweve ni mmoja wa wanafunzi shuleni hapo anasema kitendo cha shule yao kuwa na uhaba wa matundu ya vyoo kimekuwa kikiwaathiri pale tu wanapoingia kwenye mzunguko wa hedhi jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kitaaluma.

Wanafunzi hao wameomba kuongezewa vifaa vya kuhifadhia taka vitakavyotumika kuhifadhia taulo za kike ambazo zitakuwa zimetumiwa na wanafunzi.

“Sisi wanafunzi hapa shuleni ni wengi hivyo kitendo cha kuwa na matundu machache ya vyoo kinatupa wakati mgumu sana sisi wanafunzi wa kike inafika wakati tunaogopa kuka shule kwa kuhofia usalama wetu, “alisema Scolastika.

Kwa upande wake Mlezi wa wasichana shuleni hapo Shafii Mbombe amekiri kweli kuwepo kwa uhaba wa matundu ya vyoo jambo ambalo linasababisha adha kwa wanafunzi wawapo shuleni hapo.

Mlezi huyo ametoa wito kwa taasisi nyingine kusaidia tatizo hilo ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kuzingatia masomo yao ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike.

Mwanaidi Mhina ni Makamu mkuu wa shule hiyo amesema msaada waliopatiwa shuleni hapo umekuja kwa wakati muafaka ambao watoto hao walikuwa wakiuhitaji huku akionyesha umuhimu wa jambo hilo kwenye maendeleo ya kitaaluma.

Kwa upande wake Zahra Omari ambaye ni Afisa wa shirika la bima la Zanzibar kutoka makao makuu amesema kuwa maombi ya wanafunzi hao ni ya msingi kutokana na umuhimu wa vyoo kwa maisha ya jamii.

“Inakuwa, ni vigumu sana mwanafunzi anapoingia kwenye siku zake halafu akashindwa kupata huduma hiyo akapata shida ya maji na kujisaidia kwa kweli inasikitisha mno inatakiwa mwanafunzi apate hayo yote ili awe huru kuingia darasani mimi nimepokea maombi yenu na nitawasilisha panapohusika na muda mfupi Mwenyezi Mungu ajaalie mpate mnachokitaka, “alisema Zahra.

Hassan Abdalah ni meneja wa shirika la bima la Zanzibar ofisi ya Tanga amesema wamefikia hatua ya kuamua kuwasaidia wanafunzi hao taulo za kike baada ya kubainika kwamba wengi wanashindwa kuhudhuria shuleni kwasababu wanakosa huduma hiyo na kuathirika kitaaluma.

Hassan amesema shirika hilo kama mdau wa maendeleo litaendelea kusaidia wanafunzi pale ambapo itawezekana kama sehemu mojawapo ya sehemu ya faida wanayoipata.

Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo Halmashauri ya jiji la Tanga itatumia kiasi cha shilingi milioni 319 kwajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo vya walimu, wanafunzi wa kawaida na wenye ulemavu.