December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya watoto 80,000, jijini Mwanza kupatiwa chanjo ya surua rubella

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Zaidi ya watoto 80,000,wenye umri wa miezi tisa hadi miaka minne na miezi kumi na moja wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya surua rubella katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.


Hayo yamebainishwa Februari 14,2024 na Mratibu wa chanjo wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Makubi Gondera katika kikao cha kamati ya afya msingi cha Halmashauri hiyo ambacho wanakutana kupanga mikakati ya utoaji wa chanjo ya surau rubella kwa watoto katika kampeni ya kitaifa ya utoaji chanjo hiyo inayotarijiwa kutolewa kwa siku nne kuanzia Februari 15 hadi 18,mwaka huu.

Ameeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ya kitaifa ni kuzuia na kupambana na magonjwa yanayozuilika na chanjo ambayo ni surua rubella huku lengo la kampeni hiyo ni kufikia watoto kwa asilimia 100 na wameisha pokea zaidi ya dozi 85,000 ambazo wameisha sambaza ngazi ya vituo.

Pia kampeni hiyo ina lenga kuongeza kinga kwa watoto wote kwa kuwapatia chanjo hata kama ameisha pata chanjo katika utaratibu wa kawaida.

“Kinga kuu ya magonjwa haya ya surua rubella ni chanjo ambapo mtoto anapata chanjo ya kwanza anapokamilisha miezi tisa,chanjo ya pili anaipata akikamilisha miezi 18,chanjo hii ni muhimu sana hivyo tukawaelimishe wananchi wote waweze kujua umuhimu wa chanjo hii,”ameeleza Makubi.

Ameeleza chanjo hiyo itatolewa katika vituo ambavyo vitakuwa vinahama,shuleni na vituo vingine katika jamii.

“Kupitia kampeni hii anapaswa kupata chanjo ya surua rubella,surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao una athiri watu wa rika zote lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaathirika zaidi ndio maana tunawalenga wao,”ameeleza Makubi.

Aidha ameeleza kuwa dalili za mgonjwa wa surua katika siku za mwanzo kuwa na homa kali ambayo haishuki haraka,mafuta na kikohozi,macho kuwa mekundu au kutoa maji maji na vipele ambavyo vinaweza kuanza kwenye paji la uso na baadae kuenea mwili mzima.

Hata hivyo ameeleza kuwa madhara yatokanayo na ugonjwa wa surua endapo mtoto au mtu asipopata matibabu mapema ni pamoja na masikio kutoa usaha ambao unaweza kusababisha kutokusikia(uziwi),vidonda vya macho ambavyo vinaweza kusababisha upofu,remonia,utapia mlo,kuvimba ubongo na wakati mwingine asipopata huduma mapema kupata kifo.

Huku ugonjwa wa rubella na dalili zake pia zinafanana na surua unaosababishwa na virusi aina ya rubella ambao uambukizwa kwa njia ya hewa mara nyingi uwapata watoto wadogo.

Ambapo madhara ya ugonjwa wa rubella endapo mtoto asipopata matibabu anaweza kupata mtoto wa jicho, matatizo ya moyo,kutokusikia vizuri na mtindio wa ubongo pamoja na matatizo ya ukuaji ya mwili.

Makubi ameeleza kuwa mwaka 2021 kulikuwa na mlipuko wa UVIKO-19 ambayo imechangia wazazi na walezi wengi kuogopa kuwapeleka watoto kupata chanjo.

“Hili nalo limechangia watoto wengi kutofikiwa lakini tafiti zilizofanyika nchini zinaonesha kwamba ugonjwa wa rubella upo na umeathiri watoto wengi wanaozaliwa pia unaleta madhara ya kudumu kwa watoto hawa,”ameeleza Makubi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Gibson Simburia ameelezea mlipuko wa surua katika Jiji la Mwanza na maeneo mengine nchini umeisukuma serikali kutoa chanjo hiyo kwa watoto.

“Tangu 2019 mpaka leo kumekuwa na matukio ya kupokea wagonjwa wa surua miongoni mwa wananchi ambao wapo kwenye maeneo yetu na Nyamagana ikiwemo Wilaya yetu imepata wagonjwa nane mpaka sasa ambao walikuwa wanahofiwa kuwa na surua,serikali kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI na wadau mbalimbali wanakwenda kufanya kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wote wenye umri kati ya miezi tisa mpaka miaka minne na miezi kumi na moja,”ameeleza.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala amewataka wakazi wa wilaya hiyo,viongozi na wadau wengine kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo akiwemo Diwani wa Kata ya Igoma Mussa Ngollo wameomba elimu kutolewa hadi ngazi ya chini ili kufanikisha zoezi hilo pamoja na kuondoa imani potofu juu ya chanjo hiyo.