Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuanzia Julai 2023 hadi Juni 2024, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanikiwa kuwatibu utapia mlo watoto zaidi ya 100.
Hayo yamebainishwa Agosti 2,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu,wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi na uwajibikaji wa Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka huo wa fedha, kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Ambapo ameeleza kuwa jumla ya watoto 66,711 walipatiwa nyongeza ya matone ya vitamin ‘A’ huku watoto 128 walipatiwa matibabu ya utapia mlo katika kituo cha afya Buzuruga.
“Watoto wote wamepona huku jumla ya watoto 30,385,walifanyiwa tathimini ya hali ya lishe ambapo watoto 30098 sawa na asilimia 99.1 walikuwa na hali nzuri ya lishe na 284 sawa na asilimia 0.9 walibainika kuwa na dalili ya utapia mlo na watoto watatu sawa na asilimia 0.01 walikuwa na utapia mlo,”.
Hata hivyo ameeleza kuwa katika upande wa afya ya uzazi na mtoto katika kipindi cha mwaka mzima jumla ya vifo vitokanavyo na uzazi ni 8,vya watoto wachanga wa siku sifuri mpaka saba ni 38 huku vifo tisa ni vya watoto chini ya umri wa miaka 5.
Katika kuendelea kuboresha huduma za tiba Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya jumla ya chupa 3000 za damu kutoka maeneo mbalimbali.
Huku zaidi ya wananchi 56,000 walipima Virusi Vya Ukimwi(VVU), kati yao 844 walikuwa na maambukizi ya virusi hivyo ambapo wanaume ni 305 na wanawake 539.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa Halmashauri hiyo ina jumla ya vituo 65 vya kutokea huduma za afya kati ya hivyo 24 vya serikali,mashirika ya umma vinne,viwili ni vya mashirika ya kidini na 35 vya binafsi.
“Ujenzi wa zahanati nne za serikali zinaendelea,vituo viwili vipi katika hatua ya ukamilishaji Nyafura na Kawekamo huku kituo kimoja cha Nyambiti kipo katika hatua ya upauaji na cha Bwiru Press kipo hatua ya boma,”.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika