November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wananchi 200,000 kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura Kagera

Na Ashura Jumapili ,TimesMajira online Kagera

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 219,321 mkoani Kagera ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.5 ya wapiga kura zaidi ya milioni 1.4 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa Giveness Aswile katika mkutano wa tume hiyo na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani humo.

Giveness Aswile Kaimu Mkurugenzi Tume Huru ya Uchaguzi Taifa

Aswile,amesema baada ya uandikishaji Mkoa huo utakuwa na wapiga kura zaidi ya milioni 1.6 na kudai kuwa idadi inaweza kuongezeka kwa sababu inawezekana wapo Watanzania walikuwa na sifa za kuandikishwa wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 kwa sababu mbalimbali hawakuweza kujiandikisha.

Amesema Mkoa wa Kagera una vituo 1,778 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 101 kati ya vituo 1,677 vilivyotumika kwenye uboreshaji wa 2019/20.

Pia amesema mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi aina ya “BVR Kits “za sasa ambazo zinatumia programu endeshi ya android ambayo ni tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu endeshi ya windows.

Hata hivyo amesema umeanzishwa mfumo saidizi utakaowezesha wapiga kura waliondikishwa kuanzisha mchakato wa uboreshaji kwa njia ya mtandao.

“Mfumo huu online Voters Registration System ( OVRS ) kwa kutumia simu aina yotote ya mkononi au kompyuta,mpiga kura aliyepo kwenye daftari anaweza kuanzisha mchakato wa kubadili taarifa au kuhama Jimbo, Kata au kubadilisha na kuhama,”amesema Aswile.

Hata hivyo amesema mpiga kura anayerekebisha taarifa zake kwa njia ya mfumo huo shariti awe na namba ya NIDA.

Viongozi wa dini Mkoa wa Kagera wakiwa na viongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi Taifa

Baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu wamebaini wapo wapiga kura ambao wana kadi za zamani za karatasi zilizotolewa kabla ya mwaka 2015 watalazimika kwenda vituoni kujiandikisha upya maana mfumo uliotumika miaka hiyo ni tofauti na mfumo wa sasa.

Zainabu Shakiru mwakilishi wa makundi ya wanawake amesema maboresho yalitofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi ni ya mafanikio ambayo yanampa fursa kila Mtanzania ya kupata haki yake ya kupiga kura.

Shakiru anasema kitendo cha wafungwa walio na kifungo chini ya miezi 6 kupewa nafasi ya kupiga kura ni jambo jema kwa taifa kwa sababu kuwa mfungwa hakumnyimi kushiriki katika shughuli za kijamii.

Amesema kanuni za uchaguzi ni huru na haki zimegusa kila kundi zinakwenda kuweka usawa nakuonesha ukuaji wa demokrasia.

Gration Mkoba Mwenyekiti cmCHADEMA Mkoa wa Kagera t

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendelelo ( CHADEMA )Mkoa wa Kagera Gration Mkoba,amesema ni jambo jema kushirikisha wafungwa waliochini ya kifungo ya miezi 6 kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Zainabu Shakiru mwakilishi wa makundi ya wanawake katika kikao cha wadau wa uchaguzi

Mkoba pia amewataka kuangalia utaratibu wa kuandikisha wanafunzi hasa wa kidato cha sita maana zoezi la uandikishaji linafanyika wanakuwa shuleni na wakati wa uchaguzi wanakuwa wamemaliza shule na kurejea nyumbani.