Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Magu
Wananchi wa vijiji vinne wilayani Magu mkoani Mwanza wameanza kupata maji ya bomba kupitia mradi wa maji Bugando-Chabula wenye thamani ya bilioni 1.7.
Zaidi ya wananchi 12,500 wananufaika kupitia mradi huo huku wananchi wa vijiji hivyo wakiishukuru serikali kuwezesha kupatikana kwa maji ya bomba ambayo awali hayajawai kuwepo tangu vijiji hivyo kuanza.
Ambapo mradi wa maji Bugando-Chabula umetekelezwa na wataalam wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa kushirikiana na Wakala wa MajiSafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya bilioni 1.7 ili kuhudumia vijiji vya Chabula, Bugando, Nyashigwe na Kongolo wilayani Magu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA. Amos Makalla wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo,wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwajengea mradi huo ambao umekuwa msaada mkubwa katika maisha yao.
“Tunamshukuru Rais wetu kwa kutuletea mradi, hatukuwahi kufikiria kwamba tutakuwa na maji ya bomba lakini kwa jitihada za serikali sasa hivi tunapata maji bombani hii imetuondolea changamoto ya maradhi,” amesema Valentina Julius Mkazi wa Kijiji cha Chabula.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabula Masatu Mgaya, amepongeza Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mwanza kwa kutekeleza mradi huo kwa niaba ya Serikali ambao amesema umekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Daud Amlima, amesema mradi umehusisha ujenzi wa dakio la maji kutoka Ziwa Victoria, tenki la kuhifadhia maji la ujazo wa lita 250,000, vituo 31 vya kuchotea maji na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji.
Amesema kwa sasa mradi unaendeshwa na Jumuiya ya Watumiaji Maji (CBWSO) ya Nyamwaki pia mradi unatarajiwa kufikishwa kwenye vitongoji vya Dihu, Bugilang’ombe, Nyashigwe, Zuli na zahanati ya Kijiji cha Bugando.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA.Amos Makalla amesema serikali inatekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa vitendo ambapo amewasisitiza wananchi hao kuhakikisha wanalinda na kutunza mradi huo ili waendelee kunufaika sasa na hata baadaye.
Ameielekeza RUWASA kuhakikisha inasogeza huduma kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa ili kila mwananchi anayepaswa kunufaika na mradi ayashuhudie manufaa hayo kama ilivyo dhamira ya serikali.
“Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama ndoo ya maji kichwani na hapa sote kwa pamoja tunashuhudia dhamira hiyo imetimia,” amesema Makalla.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango