November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wanafunzi 400 waripoti Ilemela

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Jumla ya wanafunzi 441 kati ya 745 waliopangwa kujiunga na kidato cha tano katika shule zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wameripoti shuleni kwa ajili ya kuanza masomo kwa mwaka 2023.

Akizungumza Agosti 18, mwaka huu mara baada ya kutembelea shule ya sekondari ya wasichana ya Bwiru kwa ajili ya kukagua maendeleo ya wanafunzi wanaowasili kwa ajili ya kujiunga na kidato cha tano Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Adv.Mariam Msengi,ameeleza kuwa katika halmashauri hiyo kuna jumla ya shule tatu za serikali za kidato cha tano na sita ambapo mpaka sasa kwa shule hizo idadi hiyo ya wanafunzi wameisha ripoti shuleni.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Adv.Mariam Msengi,mwenye kitambaa kichwani,akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Kiomoni Kibamba kushoto kwake huku aliyesimama ni Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo Sylvester Murimi wakiwa na baadhi wanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari ya wasichana Bwiru.

Adv.Msengi ameeleza kuwa halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha milioni 215 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule ya sekondari ya wasichana ambapo wameweza kujenga bweni lenye uwezo wa kubeba wananfunzi 80,madarasa matatu ambayo yana samani zake ndani kwa maana ya viti na meza na matundu ya vyoo matano.

“Halmashauri yetu ina shule tatu za sekondari kwa ajili ya kidato cha tano na sita ikiwemo ya wasichana Bwiru,ya wavulana Bwiru na Buswelu ambapo tuna miundombinu ya kutosha kwa kuwahudumia wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule hizi kwa ajili ya masomo,”ameeleza Adv.Msengi.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari ya wasichana Bwiru

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Kiomoni Kibamba,ameeleza kuwa wamejenga miundombinu hiyo katika shule hiyo ili kukidhi mahitaji na kuhakikisha kila mwanafunzi aliye chaguliwa kujiunga na kidato cha tano anakuwa katika mazingira mazuri ya kupata elimu.

“Kwa shule zetu zote hakuna mtoto ambaye atabaki Rais kaupiga na anaendelea kuupiga mwingi Juni 30 mwaka huu halmashauri tulipokea kiasi cha milioni 381 kwa ajili ya kujenga sekondari mpya Kata ya Kiseke hapa tulipo Bwiru ameleta milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viliwi vya madarasa,”ameeleza Kibamba.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuishi kwa nidhamu na kuepuka vishawishi sanjari na kuishi kwa upendo,heshima na kuwaheshimu walimu pamoja na kusoma kwa bidii hadi vitabu vitoe machozi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Adv.Mariam Msengi kulia akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Kiomoni Kibamba,wakiangalia moja ya matundu ya vyoo vilivyojengwa katika shule ya sekondari ya wasichana Bwiru.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sylvester Murimi ziara hiyo lengo lake ni kukagua miundombinu,kuwakaribisha na kuwatia moyo wananfunzi wa kidato cha tano katika mafundisho yao.

Rais amesaidia kuwezesha watoto kusoma katika mazingira rafiki hivyo wazazi na walezi wawaruhusu watoto kuja mapema shuleni kwa sababu mafunzo yameisha anza na lengo ni wanafunzi kujifunza kwa wakati.

Muonekano wa nje bweni jipya kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari ya wasichana Bwiru

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana Bwiru Mecktilda Shija,ameeleza kuwa ameishukuru serikali kwa jinsi ilivyowezesha miundombinu kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha tano kwani kungekuwa na upungufu endapo wasingepatiwa fedha kwa ajili ya uboreshaji huo.

Ameeleza kuwa shule hiyo imepangiwa jumla ya wanafunzi 509 kati yao mpaka sasa 250 wameisha ripoti shuleni hapo na wanatarajia wengine kuripoti mwishoni mwa wiki hii na wiki ijayo hivyo amewahimiza kuwahi kwani Jumatatu ya Agosti 21,mwaka huu wanatarajia kuanza masomo.

“Miundombinu hii imetuboreshea sana mazingira ya ufundishaji wanafunzi 509 tuliopangiwa tunaweza kuwapokea bila upungufu wowote ,pia tumepokea kompyuta kutoka kwa ofisi ya Mbunge wetu ambazo zinaenda kuboresha ufundishaji ,”.

Vyumba viwili vipya vya madarasa kati ya vitatu vilivyojengwa katika shule ya sekondari ya wasichana Bwiru

Naye mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya sekondari ya wasichana Bwiru Kabula Julius, amemshukuru Rais kwa kuweza kuwajengea madarasa,bweni,matundu ya vyoo hivyo kuwawezesha kusoma katika mazingira mazuri na kuhaidi kusoma kwa bidii na kufika mbali.