March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wakazi 890,000 kunufaika na mradi wa maji Mto Kiwira

Na Joyce Kasiki, Dodoma

SERIKALI imeendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kusambaza maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira kwenda Jijini Mbeya, ikiwa ni hatua ya kudumu ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji katika jiji hilo.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Maji, Kundo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, aliyeitaka Serikali kueleza ni lini itakamilisha utekelezaji wa mradi huo ili kukomesha changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa Mbeya Mjini.

Akijibu swali hilo, Kundo alisema mradi huo unahusisha utekelezaji wa kazi mbalimbali zikiwemo ujenzi wa dakio na mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 117 kwa siku. Aidha, alisema kuwa matanki mawili ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa lita milioni 10 kila moja yanajengwa sambamba na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji yenye urefu wa kilometa 37.

Alieleza kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 48, na kwa mujibu wa mkataba uliopo, unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2026.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha zaidi ya wakazi 890,000 wa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi kwa kupata huduma ya uhakika ya maji safi na salama, jambo litakalosaidia kuboresha maisha na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.