November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wagonjwa 300 wapata matibabu mtoto wa jicho

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Njombe

WIZARA ya Afya imelipongeza shirika lisilo la kiserilali la Helen Keller Internationa(HKI)la Marekani kwa kugharamia kambi ya matibabu ya mtoto wa jicho kwa wagonjwa zaidi ya 300 katika wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe .

Kambi hiyo ya macho itadumu kwa wiki moja mpaka November 27 mwaka huu ambapo wananchi watakanufaika watapa huduma ya upasuaji na ,sawa na ushauri wa kitabibu .

Sarah Ludovick ni Mwakilishi wa huduma za macho Tanzania amesema ushirikiano mzuri baina ya shirika hilo na Wizara ya Afya umekuwa na tija kwani wananchi waliofikiwa na matibabu ni wale wa vijijini na wanaotoka kaya masikini.

Aidha huduma zote hizo zinafanyika katika hospitali mpya za wilaya zilizojengwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora.

Mkurugenzi wa Helen Keller International Mashariki Kusini na Kati mwa Bara la Afrika Volkan Cakir amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wagonjwa pia matibabu waliyoyapata ambao wengi wao walikuwa hawaoni lakini baada ya matibabu wamefanikiwa kuona.

“Nimefarijika namna matibabu yanavyotolewa na kwamba ushirikiano baina ya shirika na serikali umekuwa mzuri na huduma zote zinafanyika katika hospitali za serikali”alisema Cakir.

Cakir ameahidi kuendelea kutafuta wadau ili waweze kupanua wigo katika mikoa mingine kwa tatizo la mtoto wa jicho linawakumba watu wenye umri mkubwa na walio pembezoni ambao hawana kipato.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Helen Keller International Tanzania Dkt Deogratius Ngoma amesema kambi ya Wanging’ombe ni ya tano tangu kuanza mradi huu nchini na mwaka huu pekee wagonjwa elfu moja mia tatu wamenufaika na matibabu.

Ngoma amesema wamefanya kambi mbili Mkoa wa Songwe Wilaya ya Songwe na mbili Mbarali Mkoani Mbeya,moja Wanging’ombe na kambi maalumu ya watoto iliyofanyika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya jumla ya watoto kumi na tano walipatiwa matibabu.

Katika kambi ya watoto imekuwa na matokeo chanya kwani watoto wengi wameacha masomo kutokana na ugonjwa wa mtoto wa jicho na huduma hii hutolewa hospitali ya kanda kwa kuwa watoto hupewa dawa ya usingizi ambayo ni ngumu kutoa kambi za watu wazima.

Naye Dkt Simon Luvanda amesema kambi hii ni ya kwanza kufanyika Mkoani Njombe zaidi akiipongeza serikali kuboresha majengo kwani upasuaji umefanyika kwa ufanisi mkubwa kutokana na kuwepo majengo ya kisasa ashukuriwe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya.

Japhary Kisanzi(100)mkazi wa kijiji cha Ikulimambo Kata ya Uhenga Wilaya ya Wanging’ombe Mkoa wa Njombe ambaye alipatwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho zaidi ya miaka miwili amelipongeza shirika la Helen Keller International na serikali Lydia Ng’ande (76)kutoka mtaa wa Yeriko Kata ya Mdando amesema miaka miwili iliyopita alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho lakini kutokana na ukosefu wa fedha alishindwa kutibiwa.

Wagonjwa hao wameiomba serikali kuendelea kuwasaidia wananchi hasa wenye kipato cha chini ambao wengi wao wana umri mkubwa na hawana nguvu za kujitafutia kipato wengi wao wamekuwa tegemezi.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Wilaya Majaliwa Alphonse Chumvi amesema shirika la Helen Keller limefanikiwa kufanyia kambi katika hospitali hiyo kutokana na miundombinu ya majengo na vifaa tiba ni hii ni huduma ya kwanza kufanyika hospitalini hapo ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi na vifaa tiba.

Ameliomba shirika la Helen Keller International kuendelea kufanya kambi za mara kwa mara kwani uhitaji ni mkubwa.

Mpaka sasa wagonjwa mia moja sitini na tatu wamefanyiwa uchunguzi na wengine wamefanyiwa upasuaji ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kambi ya mtoto wa jicho.

Shirika la Helen Keller hugharamia uchunguzi wa awali,usafiri kwenda na kurudi hospitali,chakula,malazi,dawa na gharama za upasuaji gharama ya jicho moja kwa upasuaji ni zaidi ya shilingi laki moja na elfu hamsini.