December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya milioni 39 zimetengwa kufuatilia miradi ya maji Sengerema

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Zaidi ya milioni 39 zimetengwa kwa ajili ya kufuatilia miradi ya maji kwa Wilaya ya Sengerema,ambapo utekelezaji wake unahusisha Kata za Katunguru, Nyapande, Igalula na Nyamazuko.Huku matarajio ya wananchi katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza,ni kuona serikali ikiboresha huduma za maji.Hayo yameelezwa wakati wa mafunzo kwa wananchi ya kujengewa uwezo wa kufuatilia miradi ya serikali na Mwezeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa ufuatiliaji matumizi sahihi ya rasilimali za umma kwenye miradi ya maendeleo kutoka Chama cha Watu Wenye Ulemavu (Chawata), Adam Ndokeji,yaliofanyika wilayani Sengerema.

Ndokeji amesema matarajio yao ni kuona serikali inaboresha huduma za maji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Amesema katika mradi huo wa miezi nane, wananchi watajengewa uwezo wa kubaini miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na kuifuatilia kwa karibu.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Sengerema Allan Mhina, amewataka wananchi kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kubaini kama inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kiwango kilichokusudiwa.

“Si dhambi wananchi wakawa sehemu ya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kujiridhisha kama inatakelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa,”amesema Mhina.

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, wilaya hiyo imetengewa zaidi ya bilioni 30 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne ya maji inayotekelezwa wilayani humo.

“Miradi ni mingi na inatumia fedha nyingi za serikali, hivyo ni vyema kuwa na jicho la tatu litakalotumika kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa taarifa pale ambapo kuna watu wanaotaka kukwamisha malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi,” amesema Mhina.

Kwa mujibu wa Mhina amesema serikali ina wakaguzi wengi wanaofuatilia mradi huo ikiwemo takukuru na CAG lakini wananchi ni sehemu ya jamii itakayotumika kufanya ufuatiliaji ili kukomesha vitendo vya ubadhirifu vinavyoweza kujitokeza.

Amesema zipo changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo tabia za watu za udokoaji wa mifuko ya saruji, nondo au misumari, hivyo kuwepo kwa watu wanaofuatilia miradi hiyo watakuwa mabalozi wazuri wakupaza sauti na kutoa taarifa kwa wakati ili serikali iweze kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.

Baadhi ya wananchi kutoka wilaya ya Sengerema, wamesema mradi huo umekuja kwa wakati mwafaka ambapo huko nyuma walikuwa na maswali mengi lakini hawakuweza kupata majibu yake.Didas Msongareli amesema ipo miradi mingi ambayo mingine ilianza kutekelezwa miaka 40 iliyopita na haijakamilika.

“Wananchi hatukuwa na sautiya kuisemea kwakuwa hatukujengewa uwezo wa namna ya kufanya ufuatiliaji hivyo kupitia mafunzo haya sasa tutaanza kufuatilia kwa kina na kuripoti taarifa mbalimbali zinazoweza kupatikana kwenye maeneo hayo,” amesema Msongareli.

Kwa upande wake, Christina Edward amesema watashirikiana kwa karibuni na viongozi wa vijiji na kata ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Wananchi wakiwa kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo wa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa huduma za maji na matumizi sahihi ya fedha na rasilimali zake katika halmashauri ya wilaya ya Sengerema.