Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
BAADHI ya wananchi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga wameendelea kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) baada ya kulipwa zaidi ya milioni 125.1.
Fedha hizo ni za miezi 4 kuanzia Julai, Agosti, Septemba na Oktoba mwaka huu ambapo kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya kaya 2,602 kati ya kaya hizo 949 zitalipwa fedha taslimu zaidi ya milioni 46.3 na malipo kwa mtandao ni kaya 1,653 ambazo zitalipwa zaidi ya milioni 78.
Hayo yamesemwa Desemba 14 mwaka huu na Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Goodluck Kiboma wakati zoezi la malipo hayo kwa walengwa wa mpango huo ukiendelea.
Kiboma amesema sasa hivi wanufaika wa TASAF wanauelewa kwa sababu wanapata semina mbalimbali kabla ya malipo hayo kutoka kwa taasisi za serikali na binafsi ikiwemo benki na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Kabla ya malipo, walengwa wanapewa semina ya muda mfupi kwa mambo yanayohusu jamii inayowazunguka ikiwemo uwekaji wa akiba, kujiepusha na vitendo vya rushwa, utunzaji wa mazingira, usafi kwenye makazi yao na kujiepusha na magonjwa ya kuambukiza,” amesema Kiboma.
More Stories
Serikali yaja na mwarobaini wa changamoto ya Kivuko Magogoni – Kigamboni
Kisarawe kukata keki ya Birthday ya Rais Samia
Wataalam wa afya wakutana kujadili ugonjwa wa Marburg