Na Zena Mohamed,Timesmajira Online, Dodoma.
MAMLAKA ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA )imesema wameanza rasmi matumizi ya tiketi mtandao kwa mabasi ya masafa marefu na tayari jumla ya mabasi ya abiria 550 kati ya mabasi 47,547 yaliyopata leseni yameshaunganishwa kwenye mfumo wa tiketi mtandao.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo (LATRA ) Habibu Suluo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa shughuli za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekekezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Ambapo amesema mabasi hayo yaliyounganishwa kwenye mfumo wa tiketi mtandao kwasiku yanakatisha wastani wa tiketi 5000 hadi 7000.
“Mwaka 2021/22 idadi ya mabasi ya abiria yaliyopata leseni ni 47,547 na magari ya mizigo ni 143,011 pia zimeandaliwa njia mpya ndefu za mabasi kama vile mabasi ya kutoka Songea kwenda Mwanza na kutoka Songea kwenda Kilimamnjaro,
“Tulifanya kikao cha tathmini na baada ya kikao cha tathmini tulichofanya kwa pamoja LATRA, TRA na TABOA tumeazimia kwa pamoja kuwa kufikia mwisho wa mwezi huu wa Julai mabasi yote yawe yameunganishwa kwenye mfumo na yanatoa tiketi za kieletroniki,”amesema Suluo.
Suluo ameeleza kuwa matumizi ya tiketi za kieletroniki yamelenga kuwanufaisha wasafirishaji, abiria na Serikali.
“Kupitia mfumo huu wasafirishaji wanaweza kudhibiti mauzo ya tiketi kwa kuwa mfumo unawawezesha kuona mauzo yote yanayofanyika kupitia simu za mkononi pia matarajio yetu kuwa matumizi ya mfumo yatawawezesha wasafirishaji kuimarisha huduma zao kwa kuongeza uwekezaji kwenye sekta,”
“Lakini pia Abiria watanufaika na matumizi ya mfumo kwa kuwezeshwa kukata tiketi kutokea mahali popote na kuepukana na adha za wapiga debe,”amesema.
Amesema kuwa Serikali itanufaika kwa taarifa zinazozalishwa na mfumo kwa kupata taarifa mbali mbali zitakazosaidia kufanya maamuzi muhimu yakiwemo ya kuberesha huduma, miundombinu na kukokotoa kodi ya mapato.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo amepiga marufuku mahubiri , biashara ,mziki mkubwa na picha zisizo na Maadili kufanyika ndani ya vyombo vya usafiri na kudai kuwa vitu hivyo vinaleta kero kwa abiria na nikinyume na kanuni za usafirishaji.
“Kumekuwa na baadhi ya vyombo hivyo kukiuka kanuni za usafirishaji hivyo abiria yoyote atakayekutana na mahudhi hayo atoe taarifa kupitia namba yetu ya LATRA 0800110019 ili hatua za kisheria zichukuliwe,”amesema.
Vilevile amewataka wasafirishaji kuzingatia kanuni taratibu na miongozo ilizowekwa na Mamlaka Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) mahubiri ndani ya mabasi hayaitajiki na endapo ikabainika basi linafanya huduma hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa dereva na Mmiliki wa gari hilo.
Akizungumzia mwaka wa fedha 2022/2023 Suluo amesema LATRA imejipanga kuhakikisha kuwa huduma bora na salama za usafiri ardhini zinawafikia wananchi, kuondoa kero na changamoto mbalimbali katika sekta.
Amesema hiyo ni katika kutekeleza maelekezo anayoyatoa mara kwa mara, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Mamlaka imepanga kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 41.7 ambapo Mamlaka imejipanga kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali Shilingi Bilioni 6.3 kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na tozo za leseni na mtumizi ya mfumo wa Tiketi Mtandao.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi