December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya bilioni 1, kugharamia miradi ya kupunguza umasikini

Na Daud Magesa, Timesmajira Online Mwanza
SERIKALI wilayani Nyamagana imeeleza kuwa Jiji la Mwanza linatarajia kupokea zaidi ya bilioni 1.2 za miradi 15 ya Kupunguza Umasikini Awamu ya Nne (TPRP IV) katika sekta za elimu,afya na miundombinu barabara.

Hayo yalielezwa na Diwani wa Igoma (CCM) Mussa Ngollo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilangi wakati akifungua mafunzo kwa Kamati ya Jamii (CMC) ya usimamizi wa mradi na wajumbe wa Serikali za Mitaa (VC).

Amesema Jiji linatarajia kupokea fedha bilioni 1.24 kutekeleza miradi 15 kwa mwaka wa pili kwa kuzingatia muundo wa mradi,mitatu (3) ya ajira za muda kwa walengwa,10 ya uendelezaji miundombinu katika jamii na miwili ya kuongeza kipato cha kaya.

Ngollo amesema kwa mwaka wa kwanza Jiji la Mwanza lilishapokea jumla ya miradi 10, awamu ya kwanza miradi mitano katika kata za Igoma na Mahina,awamu ya pili pia mitano ambayo inaanza kutekeleza katika kata hizo.

Amefafanua kuwa miradi hiyo imebuniwa kupunguza athari za umasikini,ikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ngazi za jamii zilizo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Hivyo ameeleza kuwa kupitia mradi huo jamii zitatekeleza miradi ya elimu,afya na miundombinu ya barabara kwenye upungufu wa huduma hizo.

Aidha,miradi hiyo itatekelezwa katika ngazi ya kaya za walengwa wanaohudumiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kuongeza upatikanaji wa chakula,kukuza uchumi wa kaya na kupata huduma za msingi za kijamii.

Ngollo amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, Oktoba 2021 jijini Dodoma alielekeza matumizi ya fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),akieleza kwa kina umuhimu wa kuweka mkazo zaidi kutekeleza miradi ya elimu, afya, maji na kuondoa umasikini wa kipato ili kuziwezesha kaya masikini kutoka katika utegemezi.

Amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa,mkakati wa dunia nzima ni kunusuru jamii masikini na watu wa makundi maalum,umakini mkubwa wa kitaalamu unahitajika katika mradi huu kuhakikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa inaonesha thamani ya fedha na kuzingatia maelekezo yatakayotolewa.

Kwa mujibu wa Diwani huyo utekelezaji wa miradi ya TPRP jijini Mwanza itaendeleza na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli,ushirikishwaji na uwajibikaji kwa viongozi na jamii inawajibika kwa kuchangia matumizi ya nguvu kazi inayohitajika kulingana na bajeti.

Hivyo viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri wafuatilie miradi hiyo itakayowezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati na wasimamizi wa mpango wakafanye kazi kwa weledi.

Naye Ofisa Ufuatiliaji wa TASAF Jiji,Samson Kagwe ameeleza kuwa miradi ya mwaka wa pili Jiji linatarajia kupokea biilioni 1.24,limeshapokea milioni 775 za miradi husika ambapo milioni 401 za ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la zahanati ya Mahina.

Pia ujenzi wa bweni la Shamaliwa sekondari,ujenzi wa Bwalo la chakula, madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo yatakayojengwa Shamaliwa sekondari na jengo la upasuaji Mahina zahanati milioni 374.

“Mradi wa Kupunguza Umasikini awamu ya nne utawezesha kuimarisha dhana ya ushiriki wa jamii katika mchakato wa maendeleo na hivyo kuhakikisha maisha bora ya kutokomeza umasikini mkoani humu na nchi na kujiletea maendeleo yatakayowanufaisha Watanzania wote,”amesema Kagwe.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Jiji, Peter Ngagani ameeleza kuwa Kata ya Igoma haikuwa na shule ya kidato cha sita hivyo imekuwa kipaumbele cha kujenga shule ya mfano itakayokuwa darasa la watu wengine kujifunza kwa kuwa miradi yote iko eneo moja.

Amesema mafunzo yanayotolewa yataiwezesha kamati kusimamia miradi ya kijamii pia katika kutekeleza mradi huo ushiriki wa nguvu kazi ya jamii ni asilimia 10,utasaidia kuchimba msingi,kusaidia mafundi,kusomba maji na mawe.

Hivyo,jamii inaposhindwa kuchangia mradi ni changamoto,itambue mradi ni wao na si mali ya TASAF ambayo inawezesha kukamilisha tu,hivyo wachangie ikamilike ndani ya miezi mitatu na kuitunza.