December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zabuni ya kuuza mradi wa Dege bado ipo katika mchakato

Mkurugenzi Mkuu asema thamani ya Mfuko imeongezeka na fedha za wanachama zipo salama.

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Zabuni iliyotangazwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya kuuza mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni, Dar es Salaam, bado ipo katika mchakato.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mfuko kwa mwaka wa fedha 2022/23 katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.

Alisema mradi huo uliamuliwa uuzwe baada ya kufanyika tathimini mwaka 2020 na kwamba kuuzwa kwa mradi huo kutarudisha gharama zilizotumika.

“Hivi sasa tulitangaza Zabuni ambayo bado ipo katika mchakato na endapo ikatokea kwamba hatujapata mtu ambaye amefika bei ya kurudisha ile gharama maana yake ni kuwa tutatangaza tena kwa mara nyingine,” alifafanua.

Alisema kwa jinsi ambavyo wawekezaji wanavyoongezeka nchini wataweza kununua mradi huo katika kiwango ambacho kitakuwa na manufaa kwa Mfuko.

Mshomba alisema kuuzwa kwa mradi huo kutakuwa na faida kwa wanachama na Taifa kwa ujumla kwa maana kutaepusha hasara ambazo Mfuko ungepata kutokana na kuendelea nao.

Masha aliwahakikishia wanachama kuwa Mfuko upo salama na kwamba thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia shilingi trilioni 6.6 mwezi Desemba 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 36 kutoka shilingi trilioni 4.7 iliyokuwa mwezi Machi, 2021.

“Ongezeko hili linatokana na kuongeza michango ya wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji, hivyo ukuaji huu wa Mfuko unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu kwa ajili ya utoaji huduma za hifadhi ya jamii nchini,” amesema Mshomba.

Alisema katika mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni 2023, Mfuko unatarajia kukusanya michango ya shilingi trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya shilingi trilioni 1.4 kwa mwaka 2021/22.

Mshomba amesema mapato yatokanayo na uwekezaji kwa mwaka 2022/23 yanatarajiwa kuendelea kuwa shilingi bilioni 700 kiasi ambacho ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni ambapo mapato hayo yalikuwa chini ya shilingi bilioni 500.