January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini

Na Penina Malundo,Timesmajira

AFISA Tarafa wa Kata ya Kariakoo,Adrina Kishe amesema onesho la mitindo la Za Kwetu Eco Fashion Show ni moja la onesho linalofundisha jamii kuwa na uwezo wa kubuni bunifu mbalimbali kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo nchini ambazo zina ubora.

Amesema Onesho hilo limekuwa na tija kwa wabunifu na wanamitindo kujifunza ni namna gani wanaweza kubuni bunifu zenye kuleta tija kupitia mitindo.

Akizungumza hayo juzi jijini Dar es Salaam katika Onesho la mitindo ijulikanayo kwa jina la Za Kwetu Eco Fashion Show,alisema serikali itaendelea kuunga mkono miradi mbalimbali inayobuniwa na wabunifu kama hiyo ya Kimitindo ambayo inaleta tija siyo tu kwa wabunifu bali kwa jamii nzima.

Ametoa wito kwa Wabunifu na Wanamitindo kuendelea kutumia majukwaa yao ya fashion Show kuhamasisha matumizi ya bidhaa rafiki kwa mazingira na kuzalisha bidhaa zinazoheshimu utamaduni wa kitanzania.7

”Za Kwetu Eco Fashion Show siyo tu maonesho ya mitindo bali ni Jukwaa inaloonyesha uzalendo na uwajibikaji wa kijamii,tumeshuhudia vipaji mbalimbali vya wabunifu wetu wakitumia malighafi za asili na za kirafiki kwa mazingira.

”Hii ni ishara kwamba Tanzania ina hazina kubwa ya ubunifu ambayo inaweza kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”amesema.

Amesema ubunifu wa kijani ni kichocheo muhimu cha maendeleo endelevu ambapo kupitia mitindo wanaweza kufanikisha kupunguza athari mbaya kwa mazingira.

Awali akiongea katika onesho hilo wakati akimkaribisha mgeni rasmi,Mkurugenzi wa Shirika la Ladies Joint Forum(LJF)  ambao ndio waratibu wa Fasheni Show hiyo ya  Za Kwetu Eco Fashion Show,Fransisca Mboya alisema onesho hilo limeandaliwa kwa dhamira ya kukuza ubunifu,kulinda mazingira na kuimarisha uchumi wa kijani kupitia sekta ya mitindo.

Amesema LJF kama waandaaji wakuu wa onesho hilo wanaamini kwamba wanawake ni nguzo muhimu katika juhudi za maendeleo endelevu.”Kupitia jukwaa hii tunalenga kutoa nafasi kwa wabunifu hususan wanawake kuonyesha vipaji vyao na kuhamasisha matumizi ya malighafi za asili zinazojali mazingira.

”Onesho hili ni matokeo ya kazi ya pamoja kati ya wabunifu,wadau wa mazingira na wanamitindo ambao wamejitolea kuleta mabadiliko chanya katika jamii .

Amesema kupitia ubunifu wa kijana jamii inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga mustakabali bora kwa kizazi kijacho.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Onesho hilo la Za Kwetu Fashion Show,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisis ya Environmental Conservation Community of Tanzania (ECCT),Lucky Michael , amesema onesho hilo limekuwa la mafanikio makubwa kwa sababu ya ushirikiano kati ya wao na serikali.

Amesema kupitia onesho hilo kumekuwepo na ubunifu wa hali ya juu kutkutoka kwa wabunifu wa kitanzania ambao wameonyesha kwa vitendo kuwa mitindo inaweza kuwa nyenzo ya kulinda mazingira na kukuza uchumi wa nchi.