January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yazidu alia wadau kusahau ngumi Mikoani

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

BONDIA wa zamani ambae pia ni Mkufunzi wa mchezo wa ngumi, Omari Yazidu ameiomba Serikali kuhamasisha wadau wa mchezo huo kuanzisha mashindano ya ngumi katika Mikoa mbalimbali kutokana na kutokuwepo kwa hamasa jambo linalofanya upoteze muelekeo.

Yazidu ametoa kauli hiyo wakati wa kutambulisha rasmi pambano litakalofanyika Mkoani Njombe lililoandaliwa kwa kushiriana na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBRC) kupitia Rais wake Agapeter Basil ‘Mnazareth’ ili kuleta hamasa ya mchezo huo Mikoani ambapo wadau wengi wa ngumi haswa mapromota wamekuwa hawapatupii macho.

Bondia huyo aliuambia Mtandao huu kuwa, lengo la kuandaa pambano hilo ni kuibua vipaji vya mabondia wachanga katika Mikoa ambayo imekuwa haitupiwi macho na wadau wa ngumi tofauti na miaka ya nyuma ambapo mchezo huo ulikuwa unachezwa Mikoa yote ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni ambapo mapromota wamekuwa wakiandaa mapambano katika Mikoa inayotoa mabondia wakubwa kama Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.

Amesema, ni lazima sasa Kamisheni aiangalie kwani kwa sasa uendeshaji wa ngumi umekuwa ghali lakini pia kumekuwa na vikwazo vingi katika kuandaa mapambano hayo hasa yale ya mitaani ‘Gym Contest’ ambayo yameibua mabondia wengi wanaofanya vizuri hivi sasa.

“Baadhi ya mabondia wakubwa waliopa heshima nchi kama kina Francis Cheka wote wameibuliwa na mashindano hayo ambayo yalikuwa yakiibua hamasa kwani walikuwa hata wakijichangisha fedha kwenda mikoani jambo ambalo liliibua sana hamasa ya ngumi,”.

“Kwa sasa hakuna promota mkubwa atakayekubali kwenda kuandaa ngumi za aina hii kwani wanataka mabondia ambao tayari wameshaandaliwa ambao watawapa matokeo chanya katika mapambano has ana mabondia kutoka nje ya nchi,” amesema Yazidu.

Lakini pia aliishukuru TPBRC ambao wamempa kibali cha kuandaa pambano hilo baada ya kuwafuata na kuwaeleza nia yake na kuibua vipaji vya mabondia Mikoani ili kukuza mchezo wa ngumi nchini kwa kuzalisha mabondia wengi wazuri.

“Namshukuru Rais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini kwa kuniruhusu na kunipa kibali cha kuendelea kuhamasisha ngumi Mikoani ili tuendelee kuapata mabondi wengi kama kina Cheka, Mwakinyo, Kiduku kwa faida ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ngumi hazikuwa Dar, Morogoro au Tanga pekee bali ilikuwa ni kwa Mikoa yote,” amesema Yazidu.

Pia amewataka wadau na waandaaji wa mchezo wa ngumi kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo ili kuinua ngumi na kuwapa moyo mabondia wachanga wenye ndoto za kuwa wapiganaji wakubwa na Kuitangaza nchi Kimataifa.

Katika pambano hilo litakalofanyika Juni 12 kwenye ukumbi wa Mid Town, Wilaya ya Makambako bondia Barton Tweve kutoka Tunduma atapambana na Salmini Ngonyani katika pambano la Raundi 4 kilogramu 52, Fariji Pila wa Mjini Mwema Makambako na Kp Kefa kutoka Muembe Togwa watapambana katika pambano la uzani wa juu kilogramu 90 huku Stephano Wangira akizichapa dhidi ya Daniel Kamanga katika pambano la kilogramu 69.