Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KATIKA kuimarisha na kuendeleza nafasi yake kama kinara wa mapinduzi ya kidijitali nchini, Kampuni ya Mawasiliano ya Yas imezindua rasmi kampeni ya “Anzia Ulipo” visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika uzinduzi Juni 10, 2025, Mkurugenzi wa Yas visiwani Zanzibar, Aziz Ali Said amesema kampeni hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya Yas kumuwezesha kila Mzanzibari kutimiza ndoto zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“Anzia Ulipo ni zaidi ya kauli mbiu, ni mwaliko kwa kila kijana, kila mfanyabiashara mdogo, kila mbunifu kuanza pale alipo, kutumia alichonacho, na kufikia anakotamani.

“Tunaamini kuwa ndoto hazihitaji kusubiri wakati maalum au mazingira spesho; wakati sahihi ni sasa,” amesema Aziz mbele ya wadau, waandishi wa habari na washirika wa maendeleo waliohudhuria uzinduzi huo.
Katika hotuba yake, Aziz amepongeza jinsi ambavyo chapa za Yas na Mixx by Yas zilivyopokelewa kwa mikono miwili na Wazanzibari, na kuwa tayari zimetambulika kama alama ya matumaini mapya, ubunifu, na fursa visiwani humo.
Ameeleza kuwa, Yas imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu imara ya kidijitali ikiwemo mtandao wa kasi wa 4G na 5G unaopatikana kote Tanzania Bara na Visiwani, hali inayowezesha sekta muhimu kama elimu, afya, biashara na kilimo kustawi kwa kutumia teknolojia.

“Leo hii tunaona vijana wengi wakianzisha biashara zao mtandaoni, wakitengeneza maudhui ya ubunifu, wakitumia teknolojia kwenye kilimo na hata kubuni mavazi. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya miundombinu na huduma zenye tija tulizojenga,” amesema.
Kampeni ya Anzia Ulipo inalenga si tu kuhamasisha matumizi ya teknolojia miongoni mwa Watanzania, bali pia kutoa msukumo wa kisaikolojia na kimaendeleo kwa wale wanaohisi hawana mwanzo.
Kupitia huduma mahususi za Yas pamoja na bidhaa bunifu, kampeni hiyo inalenga kuwapa Watanzania silaha sahihi za kubadilisha ndoto kuwa halisi.
Aidha, Aziz amesisitiza kuwa Yas itaendelea kuwa mshirika wa karibu kwa kila Mzanzibari katika safari ya kutafuta mafanikio kupitia nguvu ya kidijitali.


More Stories
Teknolojia yawezesha wastaafu kupata huduma za PSSSF kwa urahisi
CP.Wakulyamba awataka maofisa wa NCAA kuwa wabunifu
Kipanga azindua kituo cha Mawasiliano,Serikali yaahidi elimu bora kwa Wote