March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yawaaga washindi 10 wa safari ya Dubai

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Yas,  imewaaga rasmi wateja wake 10 wanaosafiri kwenda Dubai baada ya kushinda kupitia kampeni ya ‘Tunasheherekea Pamoja – Mwaka Mmoja wa Yas’.

Hafla ya kuwaaga washindi hao, imefanyika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Yas – Kanda ya Dar Kaskazini, Aidan Komba, amesema safari hiyo ni ishara ya kuthamini wateja ambao wameendelea kuiunga mkono Yas katika kipindi chote cha ukuaji wake ndani ya mwaka mmoja.

Amebainisha kuwa, mabadiliko ya chapa yameenda sambamba na maboresho ya huduma, upanuzi wa mtandao na ushiriki mpana zaidi wa wateja kote nchini.

Kampeni hiyo, ambayo ilianza tarehe 23 Januari, imeshakabidhi zawadi kwa zaidi ya wateja 70 wakiwemo waliojinyakulia fedha taslimu, simu janja na router za 5G.

Kwa mujibu wa Komba, zawadi hizo ni sehemu ya kurudisha shukran kwa wateja wa Yas na kutambua mchango wao katika ustawi wa chapa hiyo.

Komba ameogeza kuwa, kampeni imeimarisha uhusiano kati ya Kampuni na wateja wake huku ikihamasisha matumizi ya huduma za kidijitali na uwezeshaji kwa watanzania.

Kampeni hiyo inakwenda sambamba na juhudi za kuendelea kupanua na kuboresha huduma za 4G na 5G ili kukidhi mahitaji ya kasi na nguvu ya mtandao.

Amewapongeza washindi wote 10, akisema wanaibeba chapa ya Yas wanapoanza safari hiyo.

Aidha, amekumbusha kuwa kampeni bado inaendelea na kuwataka wateja waendelee kushiriki kupitia matumizi ya huduma mbalimbali za Yas kama vifurushi vya sauti, data, intaneti na bidhaa zingine.

Amesema,  kampeni itahitimishwa kwa utoaji wa zawadi kubwa ya shilingi milioni 100.

Mmoja wa washindi, Violeth Lema kutoka Arusha, amesema, Safari hiyo ya bure anaichukulia kuwa moja ya njia nzuri ya kuwaunganisha wateja wa kutoka maeneo mbalimbali kwenda kufurahi pamoja.

Akizungumza na wanahabari amesema alipopigiwa simu kutoka huduma kutoka huduma kwa wateja ilibaki kidogo tu apuuzie simu hiyo ambayo ilimpa taarifa nzuri za ushindi wake wa safari ya Dubai.

“Nilipoona namba 100 mara ya kwanza, nilisita kupokea. Nilidhani ni simu ya kawaida tu. Lakini nilipopokea, nikaambiwa ni mmoja wa washindi. Nilifurahi sana, sikuamini kabisa,” amesema.

Ameongeza kwa kuishukuru Yas kwa kuja na Kampeni nzuri kwa ajili ya wateja wake.