Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MAMIA ya wakazi wa Jiji la Tanga na maeneo ya jirani wamenufaika na huduma ya bure ya matibabu ya macho kupitia kampeni maalum iliyozinduliwa rasmi tarehe 5 Aprili 2025 na kuendelea kwa muda wa siku tatu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Jaffari Kubecha, amewapongeza Yas kwa kuandaa zoezi hilo muhimu na kuhimiza wakazi wa Tanga kuchangamkia fursa hiyo adimu.
“Ni jambo la kupongezwa kuona taasisi binafsi zikijitoa kusaidia afya za wananchi bila malipo. Naomba wananchi wajitokeze kwa wingi kutumia huduma hii,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Pwani Kaskazini wa Yas, Abdul Ally amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za macho bila kujali uwezo wa kifedha.
“Kupitia jitihada hii, tunalenga kutoa matibabu bora na ya uhakika kwa wote, bila ubaguzi. Hili si tu ni tendo la huruma, bali ni uwekezaji katika afya na ustawi wa jamii yetu,” amesisitiza.
Huduma hiyo imetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Yas na KSI Charitable Eye Centre, ikiwa imelenga makundi maalum kama waendesha pikipiki wasiovaa kofia ngumu (helmet), watu wazima wenye matatizo ya mtoto wa jicho (cataract), wachomeleaji, pamoja na wananchi wengine wenye matatizo mbalimbali ya macho.

Naye Mwenyekiti wa KSI Charitable Eye Centre, Anver Rajpar ameelezea shukrani zake kwa Yas kwa kushirikiana nao katika mradi huo wa kibinadamu, akisisitiza kuwa afya ya macho ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Huduma zilizotolewa zilijumuisha uchunguzi wa macho, matibabu ya awali, ushauri wa kitaalamu na rufaa kwa matibabu zaidi kwa wale waliobainika kuhitaji huduma za kina.
Uzinduzi huo umeonesha dhamira ya dhati ya Yas katika kuunga mkono juhudi za serikali na sekta binafsi katika kuboresha afya ya jamii.


More Stories
Polisi kuchunguza madai ya mwanafunzi kutupa kichanga chooni
Sekiboko ahimiza uwekezaji Elimu ya ufundi
Wazee wawili jela maisha kwa kubaka na kulawiti