Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano hapa nchini, Yas, kupitia ofisi yake ya Kanda ya Kusini leo imekabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali ya Igawilo, jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaolenga kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto na mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya.
Msaada huo ambao unajumuisha vitanda vya wagonjwa, magodoro, mashuka na nepi (diapers), ni sehemu ya juhudi za Yas kusaidia taasisi za afya zinazohudumia jamii kubwa yenye uhitaji mkubwa wa huduma bora.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini, Abbas Abdurahamani ameeleza dhamira ya kampuni hiyo katika kuleta maendeleo chanya kwa jamii kwa njia endelevu.

“Afya ni eneo linalogusa kila familia, na ndiyo maana tupo hapa leo kushirikiana na watu wa Mbeya kuimarisha sekta hii muhimu,” amesema Abdurahamani.
Ameongeza kuwa, Hospitali ya Igawilo ni zaidi ya kituo cha kutolea huduma za afya, bali ni ngome ya matumaini kwa wakazi wa Mbeya na maeneo jirani. Kwa kutoa vifaa tiba, Yas inalenga kuleta mabadiliko yenye maana palipo na uhitaji wa dhati.
Akizungumza kwa niaba ya hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Igawilo, Dkt. Shaaban Mziray, aliishukuru Yas kwa msaada huo.

“Msaada huu umetufikia wakati muafaka. Utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa mama na mtoto, sambamba na kupunguza changamoto kwa watoa huduma wetu. Tunawashukuru Yas kwa moyo huu wa kipekee wa kushirikiana nasi. Hii ndiyo maana halisi ya ushirikiano wa kweli,” amesema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na wahudumu wa afya, wawakilishi kutoka Yas, wanahabari, na wageni mbalimbali.
Yas imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi za umma na jamii katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, ili kuchochea maendeleo ya pamoja, ikiwa ni muendelezo wa falsafa yao ya “Anzia Ulipo”, ujumbe unaohamasisha maendeleo kutokea pale ulipo sasa.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi