Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano Yas imeendelea kudumisha utamaduni wake wa kuungana na jamii katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuandaa futari maalum iliyofanyika katika Soko la Magomeni jana jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imehudhuriwa na zaidi ya wakazi 1,000 pamoja na viongozi wa dini, wateja na wadau mbalimbali.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo kwa niaba ya kampuni, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Dar Kaskazini, Aidan Komba, amesema futari hiyo ni sehemu ya dhamira endelevu ya Yas ya kuimarisha ukaribu na mahusiano na Watanzania, hususan katika kipindi hiki cha ibada na tafakari.
“Kipindi cha Ramadhani kinatukumbusha umuhimu wa ukarimu, mshikamano na undugu.
“Kwa kuandaa futari hii, Yas inaonyesha heshima yake kwa jamii ya Magomeni na kuthibitisha kuwa uhusiano wetu na wateja wetu unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka,” amesema Komba.
Aliongeza kuwa, kwa mwaka huu, Yas imepanga kushiriki futari na zaidi ya wateja 10,000 katika kanda mbalimbali nchini.
Lengo likiwa ni mwendelezo wa kujenga uhusiano wa karibu na wananchi wanaoiamini kampuni hiyo katika huduma za mawasiliano.
Katika kuelezea uwekezaji wa kampuni, Komba amesema Yas inaendelea kuboresha miundombinu yake ya mawasiliano nchini, ikiwa na mtandao mpana zaidi wa 4G unaofika maeneo mengi ya mijini na vijijini, pamoja na 5G katika miji ya kimkakati.
Amesema, maboresho hayo yanalenga kuwawezesha Watanzania kuwasiliana kwa uhakika, kuendesha biashara zao na kupata taarifa muhimu bila vikwazo, hasa katika kipindi cha Ramadhani ambapo mawasiliano ni jambo muhimu kwa familia na jamii.
Katika hatua ya kuunga mkono ibada za Ramadhani, Yas imezidi kuongeza thamani kwa wateja wake kupitia huduma ya Kiislamu iitwayo HIKMA.
Huduma hiyo inayotoa maudhui mbalimbali ya elimu ya dini ikiwa ni pamoja na historia ya Ramadhani, dua, mafundisho kuhusu Zakatul Fitr, Laylatul Qadr na vipindi vya ibada ya Taraweeh.
Kwa mwezi huu mzima wa Ramadhani, huduma ya HIKMA itapatikana bila malipo, ambapo wateja wanaweza kupata maudhui hayo kwa kupiga 0901655582 au kutuma SMS kwenda 15582.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Magomeni walioshiriki futari hiyo wameipongeza Yas kwa kuandaa hafla iliyowaunganisha katika imani, upendo na mshikamano.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Masoud Masoud, aliyekuwa miongoni mwa washiriki, amesema futari hiyo imeendelea kuimarisha mshikamano kati ya Yas na jamiii, na kuonyesha namna Kampuni hiyo inavyowajali wateja wake.
Hafla hiyo ya futari ni sehemu ya mwendelezo wa programu za Yas za kujumuika na jamii katika kipindi cha Ramadhani, ambapo kampuni hiyo inatarajia kuendelea na futari kama hizo katika mikoa maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam, mikoa ya Pwani, Tanga na Zanzibar.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama