March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yafanikisha utoaji huduma bure ya Macho Mwanza

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Mawasiliano hapa nchini, Yas kwa kushirikiana na Khoja Shia Ithnasheri Charitable Eye Centre iliyopo Temeke Dar es Salaam, imefanikisha utoaji wa huduma ya bure ya macho mkoani Mwanza.

Lengo la kufanya hivyo ni kupunguza changamoto za matatizo ya macho ambayo imekuwa ikiathiri watu wengi katika jamii nyingi hapa nchini.

Yas ni mdau mkubwa katika kufanikisha huduma hiyo kwa kutoa ufadhili, uratibu na kuhamasisha jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya macho mkoani Mwanza, Agosti 9 mwaka huu, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Ziwa, Joseph Mutalemwa amesema kambi hiyo ya matibabu ya macho ni sehemu ya juhudi za kulinda na kukuza afya za wananchi.

Amesema, Yas ilichagua kuangazia afya ya macho kwa sababu matatizo ya macho yanaathiri mamilioni ya Watanzania, lakini mara nyingi hayaangaliwi kwa uzito unaostahili.

“Macho ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu ambacho kinachukua takriban asilimia 80 ya taarifa zote tunazopata kutoka kwenye mazingira yetu na kutuwezesha kuepuka hatari na kuongoza miendo na kufanya kazi mbalimbali kwa usahihi.

“Hivyo kusaidia katika matibabu ya macho ni njia mojawapo ya kuwezesha Taifa, matatizo ya macho yanaweza kuathiri ubora wa maisha ya mtu.

“Hii inamaanisha kwamba kila mmoja wetu anahitaji kutambua na kutafuta msaada wa kiafya pale anapojisikia kuwa na dalili zozote za matatizo ya macho,” amesema Mutalemwa.

Aidha, amesema Kambi hiyo itatoa fursa kwa wananchi kupata vipimo, ushauri, na huduma za matibabu Bure kutoka kwa madaktari wenye ujuzi mahiri kwa muda wa siku 3 yani siku ya uzinduzi hadi leo.

Hiyo ni kambi ya 8 tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2024, ambapo imekwishafikia Watanzania zaidi ya elfu 22 katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Unguja, Pemba, Tanga, Mbeya na Dar.

Amesema, maelfu ya wagonjwa waliohitaji miwani na dawa walipewa bure, na waliohitaji kufanyiwa upasuaji pia walifanyiwa bure.

“Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwatia moyo wananchi wajitokeze kwa wingi katika kambi hii ili wanufaike na huduma zinazotolewa katika kipindi hiki cha siku 3.

“Pia, ni muhimu sana kuendelea kuhamasisha jamii zetu kuhusu umuhimu wa kuchunguza macho na kutafuta msaada wa kiafya mara wanapohisi kuwa na changamoto,” amesema.