Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya YAS, kwa kushirikiana na huduma za kifedha za kidijitali Mixx, imeungana na wadau mbalimbali wa michezo katika kuunga mkono mbio za Lake Victoria Half Marathon zilizofanyika jijini Mwanza.
Uungwaji mkono huo ni sehemu ya jitihada za kuchangia maendeleo ya jamii na kuendeleza michezo nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Ziwa, Robert Sanyagi, amesema mbio hizo hazikulenga tu ushindani wa riadha, bali zilikuwa na dhamira pana zaidi ya kusaidia watoto njiti katika hospitali za Rufaa za Sekou Toure na Bugando, ambao huhitaji uangalizi maalum ili waweze kukua na kufanikisha ndoto zao.

“Takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto 120 huzaliwa njiti kila mwezi katika hospitali hizi mbili.
“Kupitia mbio hizi, tunachangia kutoa matumaini mapya kwa familia zinazopitia changamoto za gharama za matibabu na kuokoa maisha ya vizazi vijavyo,” amesema Sanyagi.
Aidha, Sanyagi alibainisha kuwa mbio hizo zimekuwa kichocheo cha uchumi wa jiji la Mwanza, zikileta manufaa kwa mama lishe, wauzaji wa vinywaji, madereva wa magari ya usafirishaji, hoteli, pamoja na wafanyabiashara wa vifaa vya michezo na matangazo.
“Hii ni ithibati kwamba michezo si burudani tu, bali ni injini muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” ameongeza.

Kwa upande wa teknolojia, Sanyagi amesisitiza kuwa Yas na Mixx zitaendelea kutumia ubunifu na huduma zake za kidijitali kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Mtandao wetu wa 4G na 5G umewezesha wananchi wa Kanda ya Ziwa kuunganishwa kwa urahisi zaidi, huku huduma za kifedha kama Lipa kwa Simu zikirahisisha biashara kufanyika kidijitali.
“Tunaamini michezo na teknolojia vina nguvu ya kushirikiana – michezo ikijenga afya na umoja, teknolojia ikirahisisha mawasiliano na fursa,” amesema.
Sanyagi amesisitiza dhamira ya Yas na Mixx kuendelea kuunga mkono mbio za Lake Victoria Half Marathon katika miaka ijayo.
Hata hivyo amesema, mashindano hayo yamekuwa urithi wa maendeleo, mshikamano, na matumaini mapya kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na taifa kwa ujumla.

“Kwa niaba ya Yas na Mixx, nawapongeza washiriki wote. Kwa wale ambao hawajashinda leo, tambueni kwamba kushiriki ni ushindi mkubwa.
“Mmechangia kuokoa maisha na kuimarisha mshikamano wa jamii. Pamoja tunaandika historia mpya ya michezo, teknolojia na maendeleo ya kijamii,” amehitimisha.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mbio za Lake Victoria Half Marathon, Hilda Vigo, ameishukuru Yas na Mixx kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mbio hizo, akisema ushirikiano wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kukuza michezo nchini.

“Tunashukuru sana Yas na Mixx kwa kuwa sehemu ya safari hii ya mabadiliko. Mchango wao umekuwa chachu kubwa katika kufanikisha malengo ya kusaidia watoto njiti na kukuza uchumi wa Mwanza kupitia michezo. Tunatarajia ushirikiano huu kuendelea kwa miaka mingi ijayo,” amesema Vigo.
Mbio za Lake Victoria Half Marathon zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha jamii, wadau wa michezo, na sekta binafsi katika kuunga mkono maendeleo endelevu kupitia michezo na matendo ya kijamii.

More Stories
TFF yatinga na safu tatu mpya
Mkazi Kisarawe ashinda Mil. 100, Kampeni ya ‘Tunasherehekea Pamoja’
Ajinyakulia Mil. 5/- Kampeni ya Yas ‘tunasherehekea mwaka mmoja’