March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas, Mixx Wazindua Duka Jipya Dar Village Mall

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, kwa kushirikiana na Mixx, imezindua duka jipya Dar Village Mall, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kusogeza huduma karibu zaidi na wateja, sambamba na kuunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Uzinduzi huo umefanyika wakati dunia ikiadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, yenye kaulimbiu ya mwaka huu “Mission Possible”, ikiakisi dhamira ya Yas kuwa mshirika wa kweli wa Watanzania katika safari yao ya mafanikio ya kidijitali.

Kupitia duka hilo jipya, Yas inalenga kutoa huduma bora na za kisasa zaidi kwa wateja wake, ikiwemo msaada wa papo kwa papo, ushauri wa kitaalamu, pamoja na fursa ya kujifunza kwa vitendo namna teknolojia za 4G na 5G zinavyoweza kuboresha maisha ya kila siku.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Yas, Jorge Soto amesema kampuni hiyo imejipanga kuendelea kuchochea fikra bunifu miongoni mwa wafanyabiashara, wajasiriamali na watumiaji wa huduma za kidijitali ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

“Kupitia maduka kama haya, tunaleta huduma karibu zaidi na wateja wetu, tukiwapa nafasi ya kugusa, kuona na kuelewa uwezo wa teknolojia za kisasa ambazo ni msingi wa maendeleo ya kidijitali nchini,” amesema Soto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Yas na Mixx, Mwangaza Matotola amesema wiki ya huduma kwa wateja ni fursa muhimu ya kuimarisha mahusiano na wateja, na kuwasaidia kunufaika zaidi na fursa za kidijitali.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila mteja anahisi thamani yake. Kupitia duka hili jipya, tutawawezesha Watanzania kufikia huduma kwa urahisi na kwa uzoefu bora zaidi,” amesema Matotola.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mixx, Arnold Ngarashi amesema uzinduzi wa Yas Store unaakisi dhamira ya Mixx by Yas ya kuleta mageuzi ya huduma za kifedha kwa njia za kidijitali, na kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa urahisi zaidi kwa Watanzania wote.

“Kupitia Mixx by Yas, tunalenga kurahisisha maisha ya wateja wetu kwa kuwapa suluhisho bunifu za kifedha zinazoendana na mahitaji yao ya kila siku.

“Uzinduzi wa Yas Store ni sehemu ya safari yetu ya kuboresha namna Watanzania wanavyopata, kutumia na kufurahia huduma za kifedha na mawasiliano kwa pamoja chini ya mfumo mmoja wa kidijitali,” amesema Ngarashi,

Ameongeza kuwa “Tunataka kila mteja anapokutana na Mixx by Yas, ahisi urahisi, ubunifu na usalama unaoleta mabadiliko chanya katika maisha yake.”

Uzinduzi wa Yas Store katika Dar Village Mall unatarajiwa kuwa mwanzo wa mtandao mpana wa maduka ya kidijitali yatakayofunguliwa katika mikoa mbalimbali nchini, yakihimiza matumizi ya teknolojia bunifu na huduma rafiki kwa wateja.