Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Yas pamoja na huduma yake ya kifedha ya Mixx by Yas, imekutana rasmi na wateja, mawakala na wadau wa Serikali wa Kanda ya Ziwa hivi karibuni.
Wadau hao walikutana na Kampuni ya Yas katika hafla ya kipekee iliyoangazia mafanikio ya mabadiliko ya chapa na mchango wao mkubwa katika kuunganisha Watanzania na huduma za kidigitali.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amesema Yas na Mixx wameonsha mfano wa kuigwa katika matumizi ya tecknolojia ya kisasa kwa ajili ya ustawi wa wananchi.

“Mafanikio haya tunayosherehekea leo si tu ni ya kampuni, bali ni mafanikio ya Watanzania wote, hususan wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao sasa wanapata huduma bora zaidi, kwa haraka na kwa gharama nafuu.
“Natoa pongezi kwa uongozi wa Yas kwa kubuni suluhisho za kisasa zinazochochea ushirikishwaji wa kidigitali na maendeleo ya kiuchumi katika jamii yetu,” amesema Mkuu wa wilaya huyo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Ziwa, Joseph Mutalemwa amewashukuru wadau na wateja kwa kuendelea kuwa sehemu ya safari ya mageuzi ya kampuni hiyo tangu kuzinduliwa kwa chapa mpya za Yas na Mixx by Yas mnamo Novemba 26 mwaka jana.
“Kwa kipindi kifupi tangu tulipofanya mabadiliko haya, tumeshuhudia mafanikio makubwa si tu kwa kiwango cha kitaifa, bali hapa Kanda ya Ziwa ambako tumeongeza idadi ya wateja wa rika zote, kuboresha miundombinu ya mawasiliano, na kuwezesha wakazi kwa huduma bora za kidigitali kupitia teknolojia ya 4G,” amesema Mutalemwa.

Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni:
- Upanuzi wa huduma kwa wateja wote kupitia maduka ya Yas Express yaliyosambaa katika wilaya zote za Kanda ya Ziwa.
- Kuboresha huduma za Mixx kwa kuhakikisha upatikanaji wa salio kwa mawakala na kupanua matumizi ya Mixx Lipa kwa Simu kwa biashara mbalimbali.
- Kuleta mapinduzi ya maisha kwa wananchi kupitia promosheni mbalimbali ambazo zimesaidia kuibua matumaini mapya kwa Watanzania.
Aliongeza kuwa, kupitia ushirikiano wa karibu na Serikali, wadau wa sekta binafsi na jamii kwa ujumla, Yas na Mixx wamejidhatiti kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele ajenda ya ushirikishwaji wa kidigitali nchini.

“Sisi Yas na Mixx, tunaamini kuwa ni wakati wa Watanzania kutumia uwezo wao kwa njia rahisi, nafuu na ya kisasa. Tunaendelea kuwasikiliza mahitaji ya wateja wetu na kubuni njia ambazo zinatoa suluhisho ili kujenga chapa inayogusa maisha ya kila siku,” alisema.
Kwa kauli mbiu ya “Yas – Ni Wakati Wetu”, kampuni inaendelea kujenga taifa lenye wananchi waliounganishwa vyema, waliowezeshwa kidigitali, na walioko mstari wa mbele katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

More Stories
Dkt.Biteko:Tanzania yadhamiria kuendeleza mageuzi ya kidigitali katika elimu
Kikundi cha Mwanamke Shujaa chamchangia Fedha ya kuchukua Fomu Rais Samia
Magugu maji yatajwa changamoto ya uzalishaji umeme maporomoko Rusumo