Na Irene Clemence, TimesMajira Online
UONGOZI wa klabu ya Yanga umefikia maamuzi ya kumfuta kazi kocha wake mkuu, Luc Eymael kutokana na matamshi ya kibaguzi na kauli zisizo za kiungwana alizozitoa na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.
Sauti ya kjocha huyo ilianza kusambaa siku moja kabla ya mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) waliocheza jana dhidi ya Lipuli ya Iringa ambao walipata ushindi wa goli 1-0 na kumaliza msimu wakiwa nafasi ya pili.
Katika sauti hiyo kocha huyo aliwatupia lawama waamuzi na kudai kuwaonea kwa kuwanyima penalti katika mechi zao kadhaa na kusema kuwa wapo kwa ajili ya Simba na si wao.
Kocha huyo amesema kuwa, Yanga hawatakaa watwae taji la Ligi kwani si klabu bora wala timu bora, hata viongozi wa klabu hiyo ni ziro na ndio maana waamuzi wanakuwa tofauti na wao kwakuwa ni masikini hawana njia nyingine ya kulikamata Shirikisho ambalo lipo kwa ajili ya Simba na sio Yanga hivyo wamruhusu aondoke kwani hataki kubaki ndani ya klabu hiyo.
“Sifurahii katika nchi hii, watu hawajasoma, sina gari, sina Wi-fi, kufanya kazi katika mazingira haya sio kwa ajili yangu kwani hata mke wangu hafurahii, kitu pekee ninachofurahia ni pale ambapo tunacheza viwanja vikiwa vimejaa mashabiki wetu ambao nao hawajui chochote kuhusu soka. Keleleza nao nawaona kama wapuuzi kama Nyani wanavyopiga kelele au Mbwa wanavyombweka,”.
“Ni hicho tu ndicho wanachojua lakini hakuna wanachojua kuhusu soka ambalo si zuri tunapocheza ugenini kwenye viwanja vibovu ambapo maamuzi dhidi yetu, si kwa ajili yangu hii, hivyo naomba waniache niondoke baada ya mechi ya mwisho na wao wabaki na watu wao, ” amesikika kocha huyo akisema katika sauti hiyo.
Taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick imesema kuwa, kutokana na kauli hizo zisizokuwa za kiuungana, uongozi umeamua kumfuta kazi kuanzia leo Julai 27, 2020 na watahakikisha anaondoka nchi haraka iwezekanavyo.
“Uongozi unaomba radhi viongozi wa nchi, Shirikisho la Mpira wa MiguuTanzania (TFF), wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kauli za kudhalilisha zilizotolewa na kocha Luc Eymael, ” imesema taarifa hiyo.
Klabu hiyo pia imeweka wazi kuwa, wanatambua, inathamini na kuamini katika misingi ya nidhamu na utu na kupingana na aina yoyote ile ya ubaguzi.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM