Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Yanga kimefanikiwa kuendeleza ubabe kwa Watani wao wa Jadi, Simba baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 katika mchezo wao wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliochezwa leo kwenye dimba la Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Huu ni ushindi wa pili kwa Yanga msimu huu baada ya kuwafunga Simba kwa penalti 4-3 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi ‘Mapinduzi Cup’ zilizochezwa Januari 13 Visiwani Zanzibar.
Kitendo cha kushinda mchezo huo kinawafanya Yanga kuendelea kutamba msimu huu kwani wamevuna alama nne kwa Simba baada ya kutoka sare ya goli 1-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza pia ni furaha kubwa kwa mashabiki wao kwani endapo Simba wangeshinda mchezo huo basi wangetangazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu huu kupitia mgongo wao.
Pia Yanga wameendelea kuweka sawa rekodi zao kwani huo ni ushindi wao wa 38 dhidi ya Simba katika mechi 106 walizokutana ambapo Simba wameshinda michezo 31 huku wakitoka sare mara 37.
Licha ya Ushindi huo lakini bado Yanga wameshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa huo kwani hadi sasa wameendelea kusalia katika mafasi ya pili wakiwa na alama 70 walizopata baada ya kucheza mechi 32 huku Simba wakiendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi wa Ligi wakiwa na pointi 73 lakini wakiwa wamecheza mechi 30.
Sasa kazi kubwa kwa Simba ipo kwenye mchezo wao wa Julai 7 dhidi ya KMC ambapo ikiwa watashinda basi watakuwa mabingwa kwa msimu wa nne mfululizo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania