Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KLABU ya Yanga imefanikiwa kuishusha Azam na kukaa nafasi pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) baada ya kupata ushindi wa goli 3-1 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Singida United.
Ushindi huo umewafanya Yanga ambao waliingia Uwanjani huku wakitaka kupoza machungu ya kufungwa na Simba na kuondolewa kwenye mashindano ya kimataifa kufikisha pointi 67 wakiwazidi Azam alama mbili baada ya kupoteza mchezo wao wa leo jioni dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hivi karibuni kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael aliwahakikishia mashabiki kuwa mara baada ya kuondolewa kwenye mbio za kuwania nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, watahakikisha wanapambana kushinda mechi zao zilizosalia ili kumaliza msimu wakiwa nafasi ya pili.
Yanga walikuwa wa kwanza kupata goli katika mchezo huo lililofungwa dakika ya 33 na beki Paul Godfrey ‘Boxer’ ambalo ni goli lake la kwanza toka kuanza msimu huu akimalizia mpira uliogonga mwamba wa shuti la Patrick Sibomana.
Lakini wakati wakiendelea kulisakama lango la Singida, kiungo Mrisho Ngassa aliipatia Yanga goli la pili dakika ya 37 baada ya kupokea pasi safi aliyopewa na Deus Kaseke.
Kabla ya kwenda mapumziko, Singida United walipata goli
kupitia kwa Stephen Sey aliyeunganisha mpira wa kona uliopigwa na Rowadr Mshanga na kwenda mapumziko Yanga wakiongoza kwa goli 2-1.
Kipindi cha pili Yanga waliendeleza mashambulizi huku dakika ya 60 wakifanya mabadiliko ambapo mshambuliaji Yikpe Gislain aliingia kuchukua nafasi ya David Molinga.
Dakika tisa mara baada ya kuingia uwanjani, Yikpe alifanikiwa kuifungia Yanmga goli la tatu akipokea pasi ya Abdulaziz Makame na kisha kumtoka kipa Owen Chaima na kupiga mpira ulioenda moja kwa moja kwa moka wavuni.
Goli la Yikpe liliibua shangwe hasa baada ya hivi karibuni mashabiki kuonekana kutokubali kiwango anachopkionesha na kumzomea katika mechi kadhaa hali iliyosababisha benchi la ufundi kutompata katika mechi zaidi ya tatu.
Lakini wakati mashabiki wakiendelea kushangilia magoli hayo dakika ya 73 Yikpe alitaka kuwainua tena mashabiki wa Yanga baada ya kukosa kujichanga ngani ya eneo la 18 na kushinda kukwamisha wavuni pasi mpira uliotemwa na Chaima baada ya Ngassa kufanya jaribio la kufunga na hadi dakika 90 zinamalizika Singida hawakuweza kusawazisha goli hizo.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025