Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Kisarawe
WANACHAMA wa klabu ya Yanga Tawi la Mzenga Kata ya Mzenga Wilaya ya Kisarawe Mkoani, Pwani, wameuomba uongozi wa klabu hiyo na Mdhamini wao Kampuni ya GSM, kupeleka jezi na vifaa mbalimbali kwa wanaYanga wa pembezoni mwa miji mikuu.
Wamesema kuwa, wanatamani kuvinunua ili kuunga mkono klabu yao pamoja na mdhamini huyo kutokana na kazi kubwa katika kipindi kifupi, lakini wanashindwa kutokana na kutoweza kwenda katika maeneo machache yanayouzwa bidhaa hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Tawi hilo, Mohamed Rubondo amesema kuwa, kipindi kifupi tangu GSM kuanza kuidhamini klabu yao, mambo mengi makubwa yamefanyika, hivyo nao wanataka kuunga mkono juhudi hizo kwa kununua bidhaa hizo.
“Tangu Mdhamini wetu Mkuu Kampuni ya GSM kuidhamini klabu yetu, mambo mengi yanaendelea kufanyika ikiwemo usajili, sanjali na kuipeleka katika mabadiliko kujiendesha kikampuni, ambapo wanachama watamiliki Hisa, wafike huku tuiunge mkono klabu yetu,” amesema Rubondo.
Pia ameshauri liwepo gari maalumu litakalokuwa linapita katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, kuuza bidhaa hizo zikiwemo jezi, magodoro, viatu, saa na vingine vingi vinavyozalishwa na Kampuni hiyo vyenye nembo ya Yanga na visivyokuwa na nembo hiyo.
Amesema, hivi sasa klabu yao inaendelea vizuri katika ushiriki wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, na kwamba wanaimani kubwa ya kuchukua ubingwa kwa msimu huu wa 2020/2021 hivyo kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi Kimataifa.
“Tunaimani kubwa kwamba msimu huu tutautwaa ubingwa hivyo kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani, niwaombe wana-Yanga wote popote walipo tuendelee kuwapaitia ushirikiano viongozi wetu,” amesema Rubondo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania