November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yanga: Huu ni mwaka wetu wa rekodi

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

BENCHI la ufundi la klabu ya Yanga wameendelea kuipa makali safu yao ya ulinzi ili kuhakikisha msimu huu wanaweka rekodi ya kuwa timu am bayo itaruhusu magoli machache katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).

Hadi sasa katika msimamo wa Ligi, ukuta wa klabu hiyo unaoongozwa na Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Juma Makapu na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Yassin Mustapha, Kibwana Shomary, Adeyum Ahmed na Paul Godfrey ‘Boxer’ ndio uliorusu goli chache zaidi.

Mabeki hao wamekuwa msaada mkubwa kwa golikipa Mzawa, Metacha Mtana ambaye hadi sasa amejihakikishia namba baada ya kufanya vizuri katika mechi nyingingi alizocheza.

Katika mechi saba walizocheza hadi sasa na kushinda mechi sita na kupata sare moja, timu hiyo ni timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote huku wakiruhusu goli mbili pekee.

Rekodi hiyo ni bora ukilinganisha na takwimu za misimu minne iliyopita, kwani mara ya mwisho kuiona Yanga ikiwa na safu bora ya ulinzi kama hiyo ni msimu wa 2015-16, ambao katika mechi saba za mwanzoni ilikuwa imerusu mabao mawili.

Msimu uliopita wakati Yanga wamecheza mechi saba za mwanzo, walikuwa wamesharuhusu goli saba, msimu wa 2018/19 walikuwa wamesharuhusu goli nane katika mechi saba za mwanzoni.

Kupitia mtandao rasmi wa klabu hiyo, Yanga wameweka wazi kuwa wanachokitaka msimu huu ni kuweka rekodi bora zaidi ikiwemo kutoruhusu goli nyingi lakini kubwa pia ni kutaka kuongoza kwa kufunga goli nyingi.

Kwa sasa kocha mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze anahaha kuimarisha zaidi safu yake ya ushambuliaji ili kufanikisha jambo hilo baada ya kuridhishwa na kile wanachofanya safu yake ya ulinzi.

Wakiwa wanajiandaa na mchezo wao ujao dhidi ya wenyeji Biashara United ya Mara, kocha huyo pia anatumia maandalizi hayo kufanya marekebisho ya kikosi chake ili kukiongezea makali na kuwa moto wa kuotea mbali ndali ya Ligi Kuu ili kuweza kufikia malengo waliyoyaweka ikiwemo kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Kwa sasa mashabiki wa Yanga wamekuwa wakijivunia kikosi hicho kipya lakini wakiamini msimu huu hakutakuwa na ile hali ya kufungwa mabao mengi huku wakijihakikishia kuwavua ubingwa wapinzani wao.