Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa matukio ya kufanyiwa ukatili wafanyakazi wa nyumbani yamezidi kushamiri kila kukicha ambapo Juni 4, mwaka huu liliripotiwa tukio la mfanyakazi wa nyumbani Grace Joseph(17) kumwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto sehemu mbalimbali za mwili wake na mwajiri wake Christina Shiriri jina maarufu Manka kwa tuhuma za kuiba kiasi cha Tsh 161,000 licha ya kwamba aliirejesha fedha hiyo.
Kufuatia tukio hilo shirika la kutetea wafanyakazi wa nyumbani la WoteSawa limesikitishwa na kulaani kitendo cha kikatili alichofanyiwa Grace,huku likisisitiza jamii kupaza sauti juu ya vitendo hivyo na wazazi na walezi wasimamie misingi ya malezi bora na kuhakikisha wanawarithisha watoto elimu na sio kazi za nyumbani.
Tukio hilo ambalo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbroad Mutafungwa Juni 5,2024 mkoani hapa kwamba mnamo Juni 4, mwaka huu majira ya saa mbili katika Kata na Tarafa ya Usagara wilayani Misungwi Christina Shiriri alidai kuibiwa fedha zake alizokuwa amehifadhi chumbani kwake na alipomuuliza binti yake wa kazi alikiri kuchukua fedha hizo na kuamua kumrejeshea.
“Baada ya kurejeshewa fedha hizo Christina Shiriri aliamua kumfanyia ukatili binti huyo kwa kumchoma moto mikono yote miwili,tumboni pamoja na mapaja yake yote mawili,Grace amepelekwa hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya matibabu huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,”alieleza Mutafungwa katika taarifa yake alioitoa Juni 5, mwaka huu.
Akisoma tamko la kulaani kitendo hicho Ofisa Ustawi wa Shirika la WoteSawa Renalda Mambo kwa niaba ya Mkurugenzi wao Angela Benedicto,amesema baada ya kupokea taarifa hizo shirika hilo lilifanya ufuatiliaji kwenye mamlaka husika na kuweza kufika hadi Misungwi na kuongea na Mkuu wa Wilaya hiyo,Mtendaji Kata ya Nyalwigo, uongozi wa hospitali ya Wilaya hiyo ,binti mwenyewe na walezi wake ili kuthibitisha kama ni kweli tukio hilo limetokea.
Mambo ameeleza kuwa kumekuwa na wimbi la waajiri kupenda kuwaajiri watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka 14 ili waweze kuwasaidia kulea watoto wao.
“Kwa mfano mwaka 2023 tumepokea kesi 19 za watoto waliochini ya miaka 14 walioajiriwa kazi za nyumbani ,mbali na hiyo tumepokea kesi 67 za wafanyakazi wa nyumbani waliokuwa wamedhulumiwa mishahara yao,vipigo,kubakwa na mambo mengi,”ameeleza Mambo.
Pia ameeleza kuwa kumekuwa na wimbi la wafanyakazi wa nyumbani kubakwa,kuuwawa,kuchomwa moto huku akitolea mfano kuwa kuna kesi moja ya wajenzi ilitokea mkoani Morogoro waliodaiwa kumuua mfanyakazi wa nyumbani ili waweze kuiba vitu vya ndani vya mwajiri wake.
“Leo hii tunaona inaripotiwa kesi nyingine ya ukatili dhidi ya wafanyakazi wa nyumbani,ikumbukwe wafanyakazi wa nyumbani ni wasaidizi au watekelezaji wa kazi zote za nyumbani hivyo panapaswa kuwa na uhusiano mzuri kati yake na aliemuajiri ili kuepusha changamoto mbalimbali zinazowakabili ambazo zinaendelea kushika hatamu licha ya kwamba sheria ya ajira na mahusiano kazini inatambua haki za wafanyakazi wa nyumbani,”ameeleza Mambo na kuongeza kuwa;
“Tunalaani vikali vitendo vyote vya kikatili vinavyofanywa na waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani,tunapenda kuwaasa waajiri pamoja na wafanyakazi wa nyumbani wasipende kujichukulia sheria mkononi na kuacha mara moja tabia hizo ovu,”.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa waajiri na waajiriwa wanapaswa kujua taarifa sahihi kabla ya kuingia katika makubaliano ya kazi kwa kuzingatia taratibu za kisheria ili kuhakikisha familia zinakuwa salama kwa waajiri na wafanyakazi wa nyumbani kwa ujumla.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kupaza sauti dhidi ya ukiukwaji wa haki za wafanyakazi wa nyumbani na waajiri wao kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanapoona tukio lolote la ukatili au unyanyasaji katika hatua za awali kabla ya madhara makubwa hayajatokea.
Kwa upande wao viongozi wa dini mkoani hapa akiwemo Askofu Beatus Mlozi kutoka Kanisa la Waadventisti Wasabato Jimbo la Nyanza Kusini,ambaye ameeleza kusikitishwa wanaposikia matukio ya unyanyasaji, vipigo, mateso kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Ambapo ameeleza hapo ndipo pakukemea sababu halikubaliki kwa mujibu wa sheria ya nchi mtu akikosea siyo vyema kuchukua sheria mkononi ni vyema hatua za kisheria zichukuliwe haki itendeke na kila mmoja apokee adhabu kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Si vyema mtu kuchukua sheria mkononi halikubaliki,inasikitisha na mimi nailaani,ni kweli vitendo hivi vinaweza kusababishwa na binti au kijana wa kazi ambaye ametenda kosa lakini kwanini uchukue hasira,uchukue sheria mkononi bila shaka sheria itakapo shika mkondo wake wewe sasa uliyemtesa na kumtendea vitendo vya ukatili unaweza kushitakiwa,”ameeleza Askofu Mlozi.
Hata hivyo ametoa wito kwa vijana au mabinti wanaofanya kazi za nyumbani wawe waangalifu kuepuka kutenda makosa ambayo yanaweza kusababisha waajiri wao kuchukua hatua kama hizo za kuwatendea ukatili na ikitokea basi mwajiri ahakikishe anafuata sheria.
Mratibu Kamati ya Amani Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza Sheikh Twaha Bakari
ameshauri yanapotokea majambo kama hayo tuhakikishe kwamba tunafuata utaratibu wa haki na sheria za nchi pia viongozi wa dini tufanye utaratibu wa Mungu ambao ameuridhia.
“Sisi viongozi wa dini tunautaratibu binti wa ndani kama amethumiwa suala la wizi hata kiongozi wa dini hana nafasi nalo,wizi sehemu yake ni Polisi wafanye uchunguzi na kisha watafikisha mahakamani maana yake zile ni tuhuma ila sisi kwa ukatili ni kuwaweka sawa kwa kutumia maneno ya Mungu na kama ni wizi ni suala la serikali,”ameeleza Sheikh Twaha.
More Stories
Makada wa CHADEMA,mbaroni kwa tuhuma za kukimbia na karatasi za kuraÂ
Rais Samia afanya uteuzi wa viongozi mbalimbali
Chatanda aridhishwa mwitikio watu kujitokeza kupiga kura Korogwe TC